Polisi yasema makosa ya jinai yamepungua nchini
Jeshi
la Polisi nchini limetamba kushinda vita dhidi ya uhalifu baada ya
kupunguza matukio ya aina hiyo huku likikiri kuongezeka kwa vitendo vya
ubakaji na kunajisi.
Wakati
hali ikiwa hivyo, jeshi hilo limetoa tahadhari kwa watu ambao
hujihusisha na uhalifu hasa katika kipindi cha sikukuu za mwisho wa
mwaka kwa lengo la kutaka kujipatia kipato kwa njia zisizo halali kuwa
watachukuliwa hatua kali kwa kuwa limejipanga kupambana nao.
Mkurugenzi
wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Boaz, alisema hayo jijini
Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na
hali ya usalama nchini.
Alisema
hali ya usalama wa nchi kwa ujumla ni ya kuridhisha na kwamba takwimu
zinaonyesha kuwa kuanzia Januari hadi Novemba, mwaka jana, makosa
makubwa ya jinai yalikuwa 68,204 ikilinganishwa na makosa 61,794
yaliyoripotiwa mwaka huu.
Hali hiyo imesababisha upungufu wa makosa 6,410 ambayo ni sawa na asilimia 9.4.
Ubakaji Waongezeka
Hata
hivyo, Kamishna Boaz alisema makosa ya ubakaji na kunajisi yanaonekana
kuongezeka kwa kuwa kwa mwaka 2016 hadi kufikia Novemba, yaliyoripotiwa
yalikuwa 6,935 kulinganisha na makosa 7,460 ambayo yaliripotiwa mwaka
huu.
“Hili
ni ongezeko la makosa 478 sawa na asilimia 6.8 wakati makosa ya
kunajisi yalikuwa 16 mwaka 2016 ikilinganishwa na makosa 25 ambayo
yametokea mwaka huu na kufanya ongezeko la makosa tisa sawa na
asililimia 56.3,” alisema.
Alisema
kuna sababu tatu ambazo zimechangia kuongezeka kwa matukio hayo ikiwamo
mmomonyoko wa maadili kwa kuwa kuna watu wanaparamia watoto wadogo. Pia
alisema hali hiyo inachangiwa na ushirikina kutokana na baadhi ya watu
kuambiwa kuwa wakitembea na watoto wadogo wanaweza kufanikiwa katika
mambo fulani, lakini wakati mwingine hiyo inatokana na tamaa za mwili.
“Sasa
sababu hizo ni kwamba tiba yake ipo kwenye jamii na sisi tutaweka
msisitizo sana mwakani na pengine mwisho wa mwaka kuhusiana na matukio
hayo,” alisema Boaz.
Makosa dhidi ya Binadamu
Alisema
makosa dhidi ya binadamu ambayo yanajumuisha mauaji, kubaka, kulawiti
wizi wa watoto, kutupa watoto, kunajisi na kusafirisha binadamu
yaliyoripotiwa katika kipindi cha Januari hadi Novemba, 2016 yalikuwa
11,513 kulinganisha na 11,620 yaliyoripotiwa mwaka jana ambayo ni
ongezeko la makosa 107 sawa na asilimia 0.9.
Pia
alisema makosa ya wizi wa silaha, unyang’anyi katika barabara kuu,
unyang’anyi wa kutumia silaha, unyang’anyi wa kutumia nguvu, uvunjaji,
wizi, wizi wa pikipiki, wizi wa magari, mifugo pamoja na kuchoma nyumba
moto mwaka jana yaliripotiwa 34,830 wakati mwaka huu yameripotiwa makosa
29,677 ambayo ni pungufu kwa makosa 5,153 sawa na asilimia 14.8.
Makosa ya uhalifu wa kifedha
Boaz
alisema makosa ya noti bandia , wizi katika mabenki, wizi katika
mashirika ya umma, wizi katika vyama vya ushirika na makosa ya kughushi
jumla ya yaliripotiwa makosa 1,861 kwa mwaka jana ukilinganisha na mwaka
huu yaliripotiwa makosa 1,526 ikiwa ni pungufu ya makosa 335 sawa na
asilimia 18.0.
Kwa
upande wa uhalifu katika jamii, alisema makosa hayo ni yale ambayo
yanahusisha kupatikana na silaha, dawa za kulevya, bangi, mashamba ya
bangi, mirungi, nyaraka za serikali, magendo, rushwa, uvuvi haramu,
kupatikana na mazao ya bahari na wahamiaji haramu.
Alisema
makosa ya aina hiyo yaliyoripotiwa kwa kipindi cha Januari hadi
Novemba, mwaka huu yalikuwa 20,000 kulinganisha na makosa 18,971
yaliyoripotiwa mwaka jana.
Makosa ya Barabarani
Kuhusu
makosa ya usalama barabarani, alisema mwaka jana kuanzia Januari hadi
Desemba yaliripotiwa matukio 9,550 ikilinganishwa na 5,537
yaliyoripotiwa katika kipindi kama hicho mwaka huu ikiwa pungufu ya
matukio 4,013 sawa na asilimia 42.
Boaz
alisema ajali hizo zilisababisha vifo vya watu 3,108 na majeruhi 8,898
kwa mwaka 2016 wakati mwaka huu watu waliokufa ni 2,491 na majeruhi
5,696.
“Uchunguzi
umebaini kuwa kiasi kikubwa, ajali zinasababishwa na vyanzo vikuu
vitatu ambavyo ni sababu za kibinadamu, ubovu wa vyombo vya usafiri na
sababu za kimazingira.
“Sababu
za kibinadamu ni pamoja na uendeshaji wa hatari, uzembe wa madereva,
uzembe wa abiria, mwendokasi, uzembe wa watembea kwa miguu, ulevi,
mifugo isiyochungwa na uzembe wa waendesha pikipiki,” alisema.
Aidha,
alisema katika msimu wa sikukuu ya Krismasi na Mwaka Mpya, wamejipanga
vyema kudhibiti vitendo vyote vya uhalifu vitakavyojitokeza kwa kuwa
ulinzi utaimarishwa katika maeneo yote ikiwamo kwenye nyumba za ibada,
fukwe za bahari, sehemu za starehe na mengine ya mikusanyiko mikubwa ya
watu.

No comments