Mwanasiasa mkongwe nchini, Stephen Wasira ametoa siri ya kuongoza kupata
kura nyingi katika vipindi viwili tofauti katika uchaguzi wa wajumbe wa
Halmashauri Kuu (NEC) ya Chama cha Mapinduzi.
Katika uchaguzi wa NEC wa mwaka 2012, Wasira alipata kura zaidi ya 2,100
na kuwaongoza wenzake wote jambo ambalo limejirudia juzi.
Akizungumza na Mwananchi kwa simu jana, Wasira ambaye juzi aliongoza kwa
kupata kura 1,505 na kuchaguliwa kuwa mjumbe wa NEC alisema hiyo
inaonyesha jinsi wanachama wenzake wanavyomkubali ndani ya chama hicho.
Alisema anaamini mambo mengi yamechangia kukubalika kwake ndani ya chama
hicho ikiwa ni pamoja na jinsi alivyotetea msimamo wa CCM wakati wa
mchakato wa Katiba mpya.
“Wakati wa mchakato wa Katiba mpya, msimamo wa CCM ulikuwa ni Serikali
mbili, tuliamini kuwa ili kuwe na muungano imara ni lazima kuwe na
Serikali mbili, na hata mimi msimamo wangu ulikuwa hivyo,” alisema
mbunge huyo wa zamani wa Bunda.
Alisema kulikuwa na mijadala mingi ambayo iliendeshwa maeneo mbalimbali
huku CCM ikitetea msimamo wake na vyama vya upinzani vikiwa na msimamo
tofauti.
“Wakati huo nilikwenda kwenye mdahalo wa wazi pale Blue Pearl (Ubungo
Plaza). Ilikuwa ni mdahalo wa Katiba kuanzia saa tisa alasiri mpaka
12:00 jioni, nilizungumza msimamo wa chama changu na kutoa hoja za
msingi, niliwashinda Profesa Ibrahim Lipumba na Tundu Lissu,” alitamba
Wasira.
Alisema hata katika mdahalo mwingine uliofanyika katika ukumbi wa
Nkrumah, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam anaamini alifanya vizuri kuliko
Lissu ambaye alikuwa akitetea msimamo wa upinzani waliokuwa wanataka
muundo wa Serikali tatu.
Wasira alisema mchango wake mwingine ndani ya CCM ni kuongoza kamati ya
wajumbe 20 wa chama hicho kuandika ilani ya chama kuelekea uchaguzi mkuu
2015 ambayo ndiyo inatumika sasa.
“Nilikuwa mwenyekiti wa kutengeneza Ilani ya CCM, ambayo ndiyo inatumika sasa, hiyo ni ilani ya watu na nchi,” alisema Wasira.
Alisema kutokana na kukipigania chama hicho ndiyo maana wenzake wamekuwa
wakimkubali na hata kumpigia kura nyingi katika nafasi ya ujumbe wa
NEC.
Akizungumzia kushindwa kwake kutetea jimbo la Bunda na kuliacha
likiangukia mikononi mwa Ester Bulaya wa Chadema, Wasira alilaumu
alichokiita mchezo mchafu.
“Pesa nyingi ilitumika, wapinzani waliwanunua wasimamizi, mawakala,
baadhi ya viongozi wa CCM na ndiyo maana wengine wamefukuzwa,” alisema
Wasira.
“Kwa hiyo wanachama wenzangu wanataka kuonyesha dunia kuwa nilionewa na
ndiyo maana wamenipa kura nyingi. Hii kazi haina malipo, ni shughuli ya
kujitolea kwa ajili ya wanachama, lengo letu ni kujenga chama, na
wakubwa wa chama hiki ni wanachama wenyewe,” alisema.
Wasira alisema jinsi watakavyoijenga CCM, itakuwa kazi ngumu kwa vyama vya upinzani kushinda katika chaguzi zijazo.
Wasira ameshika nafasi mbalimbali katika Serikali na chama ikiwa ni pamoja na kuwahi kuwa Waziri wa Kilimo.
No comments