WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA KESHO KUFANYA MKUTANO NA WADAU WA PAMBA SHINYANGA
Waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa kesho
Ijumaa Disemba 22,2017 atafanya mkutano na wadau wa pamba kutoka mikoa
16 nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainab
Telack (pichani) amesema mkutano huo utakaokutanisha pamoja wadau wa
pamba utafanyika katika shule ya sekondari Savannah iliyopo katika eneo
la Ibadakuli manispaa ya Shinyanga.
“Mkutano huu utahudhuriwa na watu zaidi ya 1,000 wakiwemo
mawaziri,wabunge, watendaji wakuu kutoka ngazi ya
wizara,mikoa,wilaya,taasisi ,mashirika ya umma na wadau mbalimbali”,alieleza Telack.
“Serikali imedhamiria kuhakikisha kuwa wananchi wanalima zao la pamba
kwa wingi na kulifanya zao hilo lililokuwa limedorora sasa linakuwa na
tija na kuwanufaisha wakulima hivyo mkutano huu utakuwa na majibu kwa
wakulima na wadau wote”,aliongeza Telack.
Mkuu huyo wa mkoa alisema waziri mkuu pia atatembelea kiwanda cha Nyuzi
kilichopo katika kata ya Kizumbi katika manispaa ya Shinyanga.
Aidha alisema pia kutakuwa na maonesho ya biashara na shughuli mbalimbali zinazofanyika mkoani Shinyanga.
Telack alisema katika msimu huu wa kilimo cha pamba zaidi ya wakazi
80,000 wanatarajiwa kulima zao la pamba na wamepanga kulima katika ekari
67,579.9.
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainab Telack akizungumza na waandishi wa
habari leo wakati akitoa taarifa kuhusu ujio wa Waziri mkuu Kassim
Majaliwa mkoani Shinyanga
Waaandishi wa habari wakichukua matukio wakati wa kikao hicho.
Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog
No comments