Fahamu Jinsi ya Kupata Mtoto wa Kiume, Soma Hapa
KAMA wewe ni mzazi unayetamani kuwa na watoto wa jinsia uitakayo, bila shaka hii inaweza kuwa habari njema zaidi kwako.
Ni
kwamba, kuna njia kadhaa za kitaalamu zinazoweza kutumiwa na wazazi ili
kujipatia watoto wanaoweza kujiamulia kuwa wawe wa kiume au wa kike.
Uchunguzi
uliohusisha mahojiano na madaktari kadhaa wakiwamo mabingwa wa masuala
ya uzazi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, umebaini kuwa sasa wazazi
wanaweza kufanikisha ndoto ya kupata watoto wa kiume au wa kike kadri
watakavyo kwa njia rahisi inayotoa matokeo chanya kwa asilimia 80 au
nyingine ya kitaalamu zaidi inayopatikana pia nchini na ambayo matokeo
yake huwa na uhakika wa takribani asilimia 100.
Kupitia mahojiano hayo na wataalamu, Imebainika kuwa karibu wote humtanguliza Mwenyezi Mungu katika kufanikisha jambo hilo.
Akizungumza
katika mahojiano maalum yaliyofanyika Alhamisi, Daktari Bingwa wa
Wanawake katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Living Colman, alisema
jambo hilo linawezekana lakini kuna mambo muhimu ya kuzingatia kabla
wazazi kupata mtoto wa jinsia waitakayo.
Alisema
wahusika ni lazima wawe na afya njema na pia mbegu kutoka kwa mwanaume
lazima ziwe na ubora unaotakiwa katika kufanikisha utungaji wa mimba.
Kwa
mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012, Tanzania ina watu
milioni 45, huku wanawake wakiwa milioni 23, sawa na asilimia 51.
NJIA KUPATA MTOTO WA KIUME, KIKE
Wakizungumza,
baadhi ya madaktari waliitaja njia ya upandikizaji wa mbegu kuwa ndiyo
kubwa na ya uhakika zaidi kufanikisha utungaji wa mimba ya mtoto wa
jinsia waitakayo wazazi.
Hata
hivyo, Dk. Colman aliiambia gazeti hili kuwa mbali na njia hiyo
inayohusisha matumizi ya maabara, ipo njia nyingine rahisi inayotokana
na ufuatiliaji makini wa kalenda ya mzunguko wa hedhi wa mama.
“Hii
ni rahisi zaidi na haihusishi upandikizaji wa mbegu kwenye maabara…
hata hivyo, njia hii inahitaji wahusika kuwa makini zaidi katika
kufuatilia mzunguko wa hedhi wa mama kwa sababu kinyume chake matokeo
huwa hafifu,” alisema Dk. Colman.
Akieleza
zaidi, Dk. Colman alisema wengi hujaribu kufuata njia hiyo ya kalenda
na kupata matokeo hasi kwa sababu ya kutozingatia maelekezo, lakini
ukweli ni kwamba yenyewe hutoa matokeo ya uhakika kwa asilimia 80.
“Kati
ya watu 10 wanaokuja kwangu na kuomba ushauri wa namna ya kupata watoto
wa jinsi waitakayo, nane wamefanikiwa… kwa hiyo hii inawezekana
kabisa,” alisema Dk. Colman.
UFAFANUZI NJIA YA KALENDA
Wakati
baadhi ya madaktari wakitilia shaka njia ya kalenda, Dk. Colman
anasisitiza kuwa huleta mafanikio chanya kwa kiasi kikubwa na kwamba,
lililo muhimu ni kwa wazazi kuwa na utimamu wa kiafya na kubwa zaidi ni
kuzingatia muda sahihi wa kushiriki tendo la ndoa kwa nia ya kupata
mtoto.
Akifafanua,
Dk. Colman alisema daima, mwanamke huzalisha mbegu aina moja
zinazotambulika kama ‘XX’ na hizo huendeleza ukike. Kwa wanaume, mbegu
zinazozalishwa huwa ni za aina mbili ambazo ni ‘X’ (kike) na ‘Y’
(kiume).
Alisema
kuwa mbegu yoyote ya mwanamke (X) ikichavushwa na mbegu ‘X’ ya mwanaume
hutengeneza muunganiko wa ‘XX’ ambao mwishowe huwa ni kutungwa kwa
mimba ya mtoto wa kike. Hata hivyo, inapotokea mbegu ya mwanamke
ikakutana na mbegu ‘Y’ hutokea muunganiko wa ‘XY’ ambao mwishowe huwa ni
mimba ya mtoto wa kiume.
Akieleza
zaidi, Dk. Colman alisema kuwa sifa ya mbegu ‘X’ huwa ni uimara wake
kulinganisha na mbegu ‘Y’, lakini pia huwa na mwendokasi mdogo
kulinganisha na mbegu ‘Y’ ambazo zenyewe huwa hazidumu muda mrefu kabla
ya kuharibika kwa vile siyo imara kulinganisha na ‘X’, na zina
mwendokasi mkubwa zaidi.
“Mbegu
X ipo imara lakini inapotoka huenda taratibu wakati mbegu Y ni dhaifu,
lakini mwendo wake huwa ni wa kasi zaidi,” alisema.
Kwa
sababu hiyo, Dk. Colman alisema wazazi wanapaswa kuzingatia kalenda ya
mzunguko wa hedhi ili kufanikisha mimba ya mtoto wa kiume au wa kike
kulinga na na vile watakavyo.
“Ni
lazima ujue mzunguko wa mwanamke husika ni wa aina gani… kwa maana kuna
mizunguko ya wastani wa siku 28 ambayo hii yai lake hutoka siku ya 14,
kuna mzunguko mfupi wa siku 21 na yai hutoka siku ya 10 na pia wale wa
mzunguko mrefu wa siku 36 ambao yai hutoka katika siku ya 18,” alisema.
"Kwa
kawaida, yai hutoka katikati ya mzunguko wa mwanamke kulingana na
mzunguko wake. Hivyo, mbali ya kujua hilo la mzunguko, ni lazima wazazi
watambue tabia za mbegu X inayosafiri taratibu na Y inayosafiri haraka…
hilo ni muhimu kwa sababu ndilo husaidia katika kufanikisha ndoto ya
kuchagua jinsia ya mtoto," alisema.
Aliongeza
kuwa wahusika wakishiriki tendo la ndoa siku mbili au tatu karibu na
yai la mama kutoka, maana yake kutakuwa na uwezekano mkubwa wa kutungwa
kwa mimba ya mtoto wa kiume kwa vile kutokana na tabia ya mbegu Y ya
kusafiri kwa kasi, maana yake ndiyo itakayotangulia na hivyo kukutwa na
mbegu ya mama wakati nyingine ya X ikiwa imeachwa kwa vile kasi yake ni
ndogo.
Alisema
kwa sababu hiyo, wazazi wanaoota kupata mtoto wa wa kiume watalazimika
kushiriki tendo la ndoa wakati zikiwa zimebaki siku mbili au tatu kabla
ya yai la mama kutoka.
Aidha,
Dk. Colman alisema ikiwa wazazi watakuwa na ndoto ya kupata mtoto wa
kike, watalazimika kushiriki tendo la ndoa siku nyingi, kati ya 9, 10 au
11 kabla ya siku inayotarajiwa kuwapo kwa yai la mama katika mzunguko
wake.
Alisema
hilo ni muhimu kuzingatiwa kwa sababu kutokana na tabia ya mbegu X
(kike), maana yake mwendo wake utakuwa wa taratibu na itadumu kwa siku
hizo nyingi kabla ya kukutwa na kukutana na mbegu itokayo kwa mama huku
mbegu Y ikiwa tayari imeshaharibika kutokana na kutangulia kwake mbele
haraka na kukosa uimara wa kusubiria siku zote hizo.
“Mkishiriki
tendo la ndoa mapema kidogo, kama siku mbili au moja hivi karibu na yai
kutoka, mtapata mtoto wa kiume. Lakini ikiwa ni siku nyingi kabla ya
hapo kuna uwezekano mkubwa wa kupata mtoto wa kike,” alisema Dk. Colman
kabla ya kutahadharisha kwa kuongeza:
“Ila
hizi zote siyo kanuni za kudumu maana mwili wa binadamu hubadilika…
lazima hili lifanyike kwa kuzingatia mzunguko wa mwanamke na hiyo ni kwa
mujibu wa matokeo ya tafiti.”
Aidha,
Dk. Colman alisisitiza kuwa msingi wa mafanikio ya mpango huo wa
kuchagua jinsia ya mtoto kwa kuratibu mzunguko wa hedhi ya mama ni kujua
kwa usahihi siku za mzunguko huo.
“Kikubwa
ni mwanaume na mwanamke kujua yai linatoka lini ili mbegu X au Y
zikutane na yai la mwanamke na kufanikisha utungwaji wa mimba ,” alisema
Dk. Colman.
Aliongeza
kuwa, endapo kuna wazazi wanapenda kuwa na watoto wa jinsia tofauti, ni
vyema wakazingatia njia hiyo isiyogharimu chochote ya kuzingatia vyema
mzunguko wa hedhi wa mwanamke kama ni wa kawaida, mrefu au mfupi.
Alisema eneo hilo ndilo huwashinda wengi na kupata matokeo tofauti na yale wanayoyatarajia.
“Hapa
wengi huchanganya sana. Unakuta mwanamke mzunguko wake ni wa siku 28 na
hivyo yai hutoka siku ya 14, lakini wawili hao wanatumia kanuni
nyingine ya mzunguko mfupi wa siku 21 ambayo yai hutoka siku ya 10.
Ni lazima pia kuzingatia muda wa kushiriki tendo la ndoa kulingana na tabia nilizozitaja za X na Y,” alisema Dk. Colman.
“Hadi
sasa, katika watu 10 walionifuata na kuniomba ushauri wa kupata watoto
wa jinsia waitakayo, nane wamefanikiwa (asilimia 80). Kwa hiyo utaona
kwamba jambo hilo linawezekana, ila muhimu ni kuzingatia masuala hayo ya
mzunguko wa mama na siku ya kushiriki tendo la ndoa,” alisema.
NJIA YA UPANDIKIZAJI
Mbali
na njia ya kuzingatia mzunguko wa mama kabla ya kushiriki tendo la ndoa
ambayo haileti mafanikio kwa asilimia 100, Dk. Colman aliitaja njia
nyingine inayotoa fursa kwa wazazi kuchagua jinsia ya mtoto kuwa ni ile
ya upandikizaji mbegu kwa mama kuwa ndiyo ya uhakika zaidi katika
kuchagua jinsia ya mtoto.
Hata
hivyo, Dk. Colman alisema teknolojia hiyo ya upandikizaji ni ghali na
kwa hapa Tanzania bado ni ngeni na haipo katika hospitali za Serikali.
“Upandikizaji
mbegu unaanzia kwa kutolewa mbegu mwanaume na baadaye kupelekwa
maabara. Huko hupimwa magonjwa yote ili kujua ubora wake. Pia ni huko
maabara ndipo wazazi wanapoweza kujua jinsia ya mtoto wao kwa asilimia
100. Na hii ndiyo njia sahihi na ya uhakika zaidi,” alisema Dk. Colman.
Aliongeza
kuwa katika siku zijazo, anaamini kuna wakati hospitali yao (Muhimbili)
itatimiza lengo la kuanzisha Kitengo Maalum cha Matatizo ya Ujauzito na
Uzazi ambako humo, watakuwa na fursa ya kuwasaidia watu wanaohitaji
huduma ya upandikizaji wa mbegu kwa ajili ya kupata watoto.
KLINIKI YA UPANDIKIZAJI DAR
Katika
uchunguzi wake, mwandishi alipata bahati ya kutembelea kituo cha tiba
kilichoanzishwa miaka ya hivi karibuni katika maeneo ya Mikocheni jijini
Dar es Salaam kwa ajili ya kushughulikia matatizo ya uzazi huku pia
kikiwa na teknolojia ya kupandikiza mbegu kiitwacho Dar IVF and
Fertilizing Clinic.
Mkurugenzi
wa Tiba wa kituo hicho, Dk. Tamale Sali, alizungumzia pia uwezekano wa
wazazi kupata watoto wa jinsia watakayo kwa kutumia teknolojia ya
upandikizaji na kuleta matokeo sahihi ya asilimia 100.
“Tafiti
nyingi zinaonyesha kuwa hii njia ya kuchagua jinsia ya mtoto kwa
mzunguko wa hedhi hutoa matokeo ya asilimia 50 kwa 50. Siyo ya uhakika
sana kwa sababu wazazi wanaweza wanaweza kufanikiwa au wasifanikiwe.
Lakini ya upandikizaji maabara ina uhakika zaidi katika kupata mtoto wa jinsia wanayoitaka wazazi,” alisema Dk. Sali.
Akieleza
zaidi, Dk. Sali alisema kinachoweza kufanyika kwa wale wanaotaka kuwa
na watoto wa kiume au wa kike kadri watakavyo ni kuchukuliwa kwa mbegu
za mwanaume, kupelekwa maabara na huko ndiko uamuzi kuhusu jinsia ya
mtoto unaweza kutolewa na wahusika.
Aidha,
Dk. Sali aliongeza kuwa mbali na uamuzi kuhusu jinsia ya mtoto, wazazi
hupata fursa pia ya kupata mtoto asiyesumbuliwa na maradhi kama ya
kisukari na moyo.
“Mbali
ya kupimwa jinsia ya mtoto, mbegu ya baba hupimwa pia magonjwa mengine
kama ya moyo na kisukari… kama itabainika kuwa mbegu ina tatizo,
inaachwa na kuchukuliwa mbegu nyingine,” alisema.
Dk.
Sali alisema kuwa hadi sasa, tangu waanze kutoa huduma zao nchini,
tayari wameshasaidia wazazi tofauti 15 kupata watoto wa jinsia waitakayo
kwa njia ya upandikizaji huku wastani wa watoto wanaozaliwa nchini
Uganda kwa mwaka kupitia njia hiyo katika kliniki yao iliyopo nchini
humo ni 30.
Alisema
wanaopaswa kutumia njia ya upandikizaji katika kupata watoto ni
wanawake ambao mirija yao ya uzazi imeziba, wale walio na utasa na
baadhi ya wagojwa wenye uvimbe kwenye ‘ovari’, vivimbe vya vimeleo
kuzunguka mfuko wa uzazi, wanawake waliomaliza hedhi na bado wanahitaji
mchango wa mayai, waliotolewa mfuko wa uzazi lakini ovari zao zimebaki
na sababu nyingine za kijamii ikiwamo mume kusafiri kwenda masomoni au
vitani.
Alisema
kwa kawaida, wao hutoa matibabu kwa njia ya upandikizaji pale tu
inapowalazimu wanandoa kufanya hivyo ikiwa ni njia ya mwisho baada ya
njia nyingine zote za kupata mtoto kugonga mwamba.
MSIMAMO WA SERIKALI KUHUSU JINSIA ZA WATOTO
Baadhi
ya watu hutamani kuwa na mchanganyiko wa jinsia katika orodha ya watoto
wao na hivyo huwa tayari kufuata njia mbalimbali ili kuwapata watoto wa
jinsia waitakayo ili kukidhi matakwa yao.
Hata
hivyo, imebainika kuwa baadhi ya njia haziruhusiwi nchini ikiwamo ile
ya kukatisha uhai wa mimba ya mtoto wa jinsia wasiyoitaka wazazi wakati
wa kutungwa kwake.
Mkurugenzi
wa Uhakiki wa Ubora wa Huduma katika Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Mohamed Mohamed, alisema ni kosa kisheria
kwa mama kutoa mimba baada ya kujua jinsia ya mtoto anayetarajia kumzaa.
Kuhusu
upandikizaji alisema sheria inatambua wale wenye matatizo ya uzazi,
wenye umri mkubwa na ukomo wa hedhi kuwa hawakatazwi kupandikiza lakini
siyo wanandoa wenye afya njema na uwezo wa kupata watoto kwa njia ya
kawaida.

No comments