Kakobe ainyambua taarifa ya TRA
Siku sita baada ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutoa taarifa ya
uchunguzi katika Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF), Askofu
Mkuu wa kanisa hilo, Zachary Kakobe ameibuka na kuipangua huku
akiishangaa taasisi hiyo ilivyoanika barua yake ya siri aliyomwandikia
Rais John Magufuli.
Akizungumza jana katika kanisa hilo lililopo Mwenge, jijini Dar es
Salaam, Askofu Kakobe aliyekuwa akishangiliwa mara kwa mara na waumini
wake alianza moja kwa moja kujibu taarifa hiyo ya TRA mara tu baada ya
kupanda madhabahuni kuanzia saa 7:14 mchana hadi saa 10:7 jioni, “Yapo
mambo kadhaa yaliyopotoshwa ambayo yanatakiwa kunyooshwa,” alianza.
“Swali linakuja, kwa nini watu hawa miaka yote walikaa kimya leo
wanaibuka na kusema kanisa langu linakwepa kodi? Taarifa hii ni ya
kishilawadu, kisiasa na inayolenga kunichonganisha na waumini wangu.”
Shilawadu ni kipindi kinachorushwa na televisheni ya Clouds kila siku ya
Ijumaa, kikizungumzia zaidi maisha binafsi ya wanamuziki, wasanii na
watu maarufu.
TRA ilifanya uchunguzi huo kutokana na kauli ya Askofu Kakobe aliyoitoa
alipozungumza na waumini wake katika mkesha wa Krisimasi mwishoni mwa
mwaka jana kwamba ana fedha kuliko Serikali.
Baada ya kauli hiyo, Kamishna Mkuu wa TRA, Charles Kichere alisema watafanya uchunguzi kubaini utajiri huo.
Baadhi ya mambo ambayo Kichere alieleza TRA kuyabaini baada ya uchunguzi
huo ni; Askofu Kakobe kutokuwa na akaunti wala fedha katika taasisi
yoyote ya fedha nchini zaidi ya kuwa mmoja wa wasimamizi wakuu wa
akaunti ya kanisa, akaunti za kanisa zipo katika Benki ya NBC zikiwa na
zaidi ya Sh8 bilioni.
Nyingine ni kanisa hilo kukwepa kodi ya Sh20 milioni, kampuni
inayomilikiwa na watoto wa Askofu Kakobe ilikwepa kulipa kodi ya Sh37
milioni ambazo zote zimelipwa baada ya uchunguzi.
Nyingine ni kanisa hilo kutunza kiasi kikubwa cha fedha kwenye ndoo na
majaba kinyume cha utaratibu wa utunzaji fedha, uwekaji na utoaji wa
fedha nyingi benki bila ya kushirikisha vyombo vya ulinzi pamoja na
fedha za kanisa kutumika kujenga nyumba ya mke wa Askofu Kakobe kwa jila
lake badala ya kanisa, jambo ambalo ni kinyume na utaratibu wa kanisa.
Pia, Kichere alieleza kuwa Askofu Kakobe alimuandikia barua Rais
Magufuli kuomba radhi kutokana na kauli yake ya kebehi pamoja na
matamshi yake ya dharau kwamba ana fedha nyingi kuliko Serikali.
Majibu ya Kakobe
Huku akizungumza kwa makini, Askofu Kakobe alianza kwa kuzungumzia barua
iliyoelezwa na TRA kwamba alimuomba radhi Rais, “Kwanza nashangaa, mimi
niliandika waraka wa kichungaji wa siri kwa Rais juu ya mambo kadha wa
kadha nikimpongeza kwa kazi yake na niliandika kwa heshima iliyotukuka.”
Alisema barua hiyo aliandika bila kuwashirikisha wasaidizi na waumizi
wake, kwamba kitendo cha TRA kuiweka wazi kimemsikitisha kwa sababu
mamlaka hiyo si msemaji wa Rais.
“Siwezi kuomba radhi wala msamaha kwa mtu wa aina yeyote.
Nilichokiandika katika waraka kwa Rais ni sauti ya Mungu, kama wanataka
wamwambie Mungu aombe msamaha si Kakobe. Mungu ndiye aliyezungumza.”
Kuhusu uchunguzi wa TRA, alisema baada ya taarifa hiyo kutolewa aliamua
kukaa kimya licha ya watu kumtaka ajibu kwa sababu katika kipindi hicho
kulikuwa na mambo muhimu ya kitaifa yaliyokuwa yakijadiliwa.
“Ningejibu wakati ule majibu yangu yangekuwa habari kubwa, kwa sasa
ninaweza kuzungumzia taarifa ya TRA,” alisema Kakobe huku akiuchambua
uchunguzi huo wa TRA.
“Kamishna wa TRA alishukuru namna nilivyompa ushirikiano mzuri juu ya
uchunguzi wao. Walitumia nguvu kubwa kuchunguza na walithibitisha kuwa
sina fedha katika taasisi yoyote ile. Sina mradi, sina shamba wala
sifugi hata panya.”
Alisema katika uchunguzi huo, TRA walibaini kuwa mke wake hana mradi
wala fedha zozote kwenye taasisi na kwamba aliwaeleza fedha alizonazo
zinatokana na wito wake kama walivyo watu wengine.
“Katika taarifa yao kuna mambo mengi yaliyopotoshwa, sina uhakika kama
ni kwa makusudi. Mnakumbuka Januari 14 siku ya Jumapili kama leo (jana)
niliwaeleza kuwa kuna njama na hila zinazopangwa juu ya kupotosha ukweli
wa mambo,” alisema.
Alisema TRA walikwenda nyumbani kwake na kanisani kufanya upekuzi hadi
chumbani kwake, “Nikawaeleza atakayeona kitu chochote kinachoashiria
mimi ninakwepa kodi basi nitampa zawadi.”
Alisema maofisa wa TRA pia walibaini kuwa kanisa lake ni safi na halina
shida yoyote na kusema alishangaa jambo hilo kutoandikwa katika taarifa
ya mamlaka hiyo.
“Walishangaa ninaishi katika nyumba ambayo haifanani na hadhi yangu na
heshima kubwa niliyonayo. Walisema sifai kuishi katika nyumba hiyo kwani
si ya kiwango changu,” alisema.
Alisema kutokana na hilo, maofisa hao walitoa ushauri kwa washirika wa
kanisa lake, kwamba mpango walionao wa kumjengea nyumba ufanyike haraka
ili aweze kutoka katika nyumba anayoishi sasa.
“Waliyozungumza kwenye taarifa yao yanachanganya. Mfano, wamesema kanisa
hili lina akaunti kwenye benki ya biashara (NBC) na kutaja kiasi cha
fedha katika akaunti wakati ni kinyume na sheria za kibenki,” alisema.
Alisema akaunti hiyo ipo tangu miaka ya 1990 na kwamba taarifa ya TRA
imemsikitisha yeye na waumini wake na kumfanya aamini kuwa uchunguzi
dhidi yake umefanyika kisiasa, si kisheria.
“Wamesema tuna akaunti benki ya biashara, wakasema na kiasi kilichopo
lakini wakati huohuo wanasema tuna fedha tumehifadhi kwenye ndoo na
majaba,” alisema na baadhi ya waumini kuitikia, “Ni siasa hizo.”
“TRA wamesema fedha zilizoko benki zina wasimamizi sita ma-signatory
(watia saini) mimi nikiwa msimamizi mkuu wa fedha hizo. Sasa najiuliza
mimi ni msimamizi wa fedha za benki au za kwenye ndoo na majaba.”
Wakati Kakobe akieleza kuhusu ndoo na majaba, waumini walikuwa wakinyoosha juu ndoo na majaba hayo.
“Sasa wanataka sadaka zikusanywe kwenye khanga na vitenge? Kazi ya ndoo
hizi ni kukusanya fedha zinazotolewa na waumini kanisani kama ilivyo
makanisa mengine na baada ya hapo fedha hizo hukusanywa na kupelekwa
benki,” alisema.
Alidai kwamba alishaonyeshwa na Mungu kwamba uchunguzi huo wa TRA dhidi
yake lengo lake ni kumchonganisha na waumini wake, kuwataka wazipuuze.
“Kunichonganisha mimi na nyinyi hiyo ni biashara ya kichaa. Majaribio
haya yamefanyika kwa zaidi ya miaka 10 lakini hawakufanikiwa,” alisema
Kakobe.
Alisema waumini wake wanamuamini kuliko wanavyowaamini wazazi wao na kwa
heshima huwa wanamuita baba na wanaogopa kumuita Kakobe.
“Ni rahisi kuwachonganisha waumini wangu na wake zao au waume zao lakini
si kuwachonganisha na baba yao (Kakobe).Wangapi wananiamini,” alihoji
na kujibiwa na waumini hao huku wakinyoosha mikono juu na kupiga makofi.
Kuhusu kusafiri na mkewe nje ya nchi, Askofu Kakobe alisema, “TRA
wanalalamika kuwa natumia fedha vibaya kwenda nje na familia yangu. Hili
jambo si kweli.”
Aliwaita madhabahuni waumini wake waliowahi kusafiri nje ya nchi kwa
fedha za kanisa na kuwapa kipaza sauti na kutaja nchi walizowahi kwenda.
“Sasa hawataki nisafiri na mke wangu kwenda nje ya nchi wanataka
nisafiri na changudoa? Hawajui kuwa mke wangu ndio mlinzi, hata
changudoa akigonga mlango mke wangu ataamka na kwenda kumfungulia,”
alisema.
Kuhusu fedha zilizokuwa zimewekwa kwenye kampuni iliyowahusisha watoto
wake, alisema zilikuwa fedha ambazo waumini wake walichangisha kwa ajili
ya kumjengea nyumba na ziliwekwa katika akaunti nyingine ili wapate
riba.
“Zilivyofikia malengo, zilitolewa na kuingizwa katika akaunti ya kanisa.
TRA walisema zilitolewa bila kufuata utaratibu na hazijalipiwa kodi.
Tuliamua kuzilipa hizo fedha,” alisema.

No comments