Kiongozi wa Chadema Kuagwa Leo na Kusafirishwa Iringa kwa Maziko
VIONGOZI mbalimbali wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),
wanatarajia kuhudhuria mazishi ya aliyekuwa Katibu wa Chama hicho kata
ya Hananasifu, Daniel John.
Daniel alikutwa amefariki dunia kwenye ufukwe wa Coco, Manispaa ya
Kinondoni jijini Dar es Salaam huku mwili wake ukiwa na majeraha na
inadaiwa alitekwa na watu wasiojulikana akitokea katika shughuli za
kampeni za uchaguzi wa marudio wa Jimbo la Kinondoni.
Taarifa kutoka kwa Mkuu wa Idara ya Mawasiliano wa chama hicho, Tumaini
Makene, jana ilieleza kuwa mwili wa marehemu John unatarajiwa kuzikwa
kesho mkoani Iringa.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa mwili utapelekwa Kanisa Katoliki Hananasifu
kwa ajili ya misa ya kumuombea marehemu itakayoanza saa 5.00 asubuhi.
“Viongozi wa chama, wakiwemo wakuu na waandamizi, wanatarajiwa kuongoza
shughuli ya utoaji wa heshima za mwisho kwa mwili wa aliyekuwa Katibu wa
Chama Kata ya Hananasifu, Jimbo la Kinondoni, Kamanda Daniely John,
itakaofanyika kesho (leo), jijini Dar es Salaam,” alisema Makene.
Alisema baada ya ibada, waombolezaji watatoa heshima za mwisho na
baadaye mwili kusafirishwa kwenda mkoani Iringa ambako atazikwa katika
kijiji cha Chikelewatu wilayani Mafinga.
Aidha, Chadema imetoa wito kwa wanachama wa chama hicho kujitokeza kutoa heshima zao.
Juzi, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni aliweleza
waandishi wa habari kuwa uchunguzi wa tukio la kuuawa kwa kada huyo wa
Chadema unaendelea vizuri, na kwamba hadi sasa Jeshi la Polisi
limeshamkamata shahidi mmoja ambaye anatoa ushirikiano mzuri.
Masauni alisema pindi uchunguzi utakapokamilika, taarifa itatolewa kwa
wananchi ili wafahamu ukweli wa tukio hilo ambalo limeleta sintofahamu
kwa jamii.

No comments