Mtangazaji mmoja wa redio nchini Marekani amejifungua akiwa hewani wakati wa kipindi chake cha alfajiri.
Cassiday Proctor, mtangazaji wa kipindi cha redio cha alfajiri katika
kituo cha redio cha The Arch katika mji wa St Louis nchini Marekani
alitangaza kujifungua kwake kupitia njia ya upasuaji siku ya Jumanne.
Bi Proctor alianza kuhisi uchungu wa kujifungua siku ya Jumatatu .Kituo
chake cha habari kilishirikiana na hospitali ambayo alijifungua ili
matangazo yake kwenda moja kwa moja hewani.
Aliambia BBC kwamba alipata fursa ya kwenda hewani moja kwa moja
alipokuwa akijifungua mtoto huyo wiki mbili kabla ya muda uliotarajiwa.
''Ilikuwa furaha kuweza kuwa hewani na wasilikizaji wetu katika siku
muhimu ya maisha yangu'' , alisema bi Proctor kuhusu kipindi hicho.
Alisema kuwa kujifungua ukiwa hewani ni mwendelezo ya kile
kinachoendelea kila siku katika kipindi hicho ,''mimi huwaambia
watazamaji wangu kila kitu kinachoendelea katika maisha yangu.'' .
Mtoto huyo aliyekuwa na uzani wa 7lbs 6oz amepatiwa jina Jameson baada
ya wasikilizaji kupendekeza jina la mtoto huyo katika shindano mwezi
Januari.
Majina 12 ya kijinga pamoja na mengine 12 yaliochaguliwa na mtangazaji huyo na mumewe yaliwekwa katika sehemu moja .
''Tulipiga kura hadi tulipopata Jameson'', alisema mkurugenzi wa vipindi Scott Roddy .
Mtangazaji mwenza wa bi Proctor Spencer Graves aliambia BBC kwamba hatua hiyo ya kujifungua hewani ilikuwa ya kipekee.
No comments