Simanzi yatawala mwili wa kada wa chadema aliyeuwa kwa kutekwa
Simanzi na vilio vilitawala wakati wa
ibada ya kuuaga mwili wa aliyekuwa kada wa Chama cha maendeleo na
Demokrasia (Chadema), Daniel John, aliyeuawa na watu wasiojulikana.
John aliuawa wiki iliyopita katika
ufukwe wa Bahari ya Hindi, eneo la Coco wakati akitokea katika kampeni
za uchaguzi mdogo wa marudio jimbo la Kinondoni na mwili wake uliokotwa
katika ufukwe wa Coco.
Wakati mambo yakiwa hivyo katika ibada
hiyo iliyofanyika kwenye Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu Anna
Hananasif, Kinondoni jijini Dar es Salaam, Jeshi la Polisi liliwazuia
wafuasi wa Chadema waliotaka kuusindikiza mwili kwa kuusukuma hadi
barabara ya Kawawa Kinondoni.
Ibada ya kuuaga mwili wa John, aliyekuwa
Katibu wa chama hicho kata ya Hananasif, ikongozwa na Paroko Alistadius
Kibangula, viongozi mbalimbali wa Chadema wakiongozwa na Mwenyekiti wa
Chadema Kanda ya Pwani na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye,
walihudhuria.
Viongozi wengine waliohudhuria ni pamoja
na Makamu Mwenyekiti Chadema Taifa, Prof. Abdalah Safari, Meya wa
Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob.
Akizungumza baada ya ibada, Sumaye alisema chama kimesikitika kwa yote yaliyotokea dhidi ya John.
"Daniel hakufariki (dunia) kwa sababu ya
kupigania Chadema, bali alifariki kwa kupigania haki ya Watanzania.
Wapo wengi ndani ya Chadema waliofariki dunia kwa kupigania haki,”
alisema Sumaye.
Alisema anaamini serikali itafanya
uchunguzi pamoja na kutenda haki kwa wote waliohusika na kifo cha
Daniel.Naye, Meya Jacob alisema Daniel alikuwa mtaalamu wa siasa za
mtaani, na aliishi na watu vizuri.
“Marehemu ndiye aliyechangia ushindi wa
Chadema katika uchaguzi wa mwaka 2015 kwa kupata Diwani na Mbunge. Yeye
pia ndiye aliyeisambaratisha CCM kata ya Hananasif iliyokuwa inaongozwa
na Tarimba,” alisema Jacob.
Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi lililazimika kuwazuia wafuasi wa Chadema, waliotaka kuusindikiza mwili wa John.
Baada ya ibada ya kuaga mwili katika
Kanisa hilo, wafuasi wa Chadema walijipanga kwa ajili ya kulisindikiza
kwa kulisukuma gari lililobeba mwili wa marehemu John lakini walipofika
mtaa wa Tarimba eneo la Kinondoni Muslim, walizuiwa na askari waliokuwa
kwenye magari mawili ya wazi.
Askari hao walikuwa katika magari yenye
namba PT 3675, pamoja na PT 1686 yote aina ya Toyota Land Cruizer.
Polisi hao waliwazuia wafuasi hao na gari lililobeba mwili kuendelea na
safari.


No comments