Mbunge wa jimbo la Kigoma Mjini , Mhe. Zitto Kabwe amefunguka na kudai
kuwa jeshi la polisi nchini limekuwa likikiuka utaratibu na kuvunja
sheria na kusema akiwa rumande amemshuhudia kijana ambaye amevunjwa
mbavu kituoni na hajapelekwa kutibiwa.
Zitto Kabwe amesema hayo leo Februari 24, 2018 akiongea na waandishi wa
habari na kusema kuwa kitendo cha yeye kukamatwa na kulazwa ndani kwa
siku moja kumemfanya agundue kuwa kuna Watanzania wengi wanateseka na
kupata shida kwenye vituo vya polisi nchini.
"Watanzania wanateseka sana chini ya mikono ya polisi, sheria inataka
ndani ya masaa 48 polisi wame wamewafikisha mahakamani watuhumiwa lakini
tumekutana na watu wamekaa ndani siku 3 hata maelezo tu hawajaandika,
wengine wana siku 20 wapo ndani hawajafikishwa mahakamani" alisema Zitto
Kabwe
Kiongozi huyo aliendelea kudai kuwa polisi wamekuwa wakiwatesa wananchi
ndani ya vituo hivyo vya polisi na kusababisha majeraha kwa baadhi ya
watuhumiwa bila kuwapeleka hospitali kwa matibabu.
"Tumekuta watu ambao wanateswa, kijana mmoja mpaka mbavu zimevunjika na
zaidi ya siku saba hajapelekwa hospitali kwa matibabu, mpaka jana
tunaondoka hajapelekwa hospitali, tulipozungumza na Kamanda wa Polisi
Mkoa wa Morogoro tulimweleza hilo, kuna watu ni wagonjwa hawajapelekwa
hospitali akasema atashughulikia sasa sijui kama yeye alikuwa hajui
hilo" alisema Zitto Kabwe
Mbali na hilo Zitto Kabwe amesema hali kiujumla ya nchi yetu kwa sasa ni
tata kwa kuwa suala la mauaji yameendelea kutokea kinyume na mazoea
yaliyokuwepo kipindi cha nyuma na kudai kuwa kuna kila sababu ya
uchunguzi wa mauaji hayo kuanzia yale ya Kibiti mpaka haya ambayo
yanaendelea sasa kuchunguzwa na vyombo huru na si jeshi la polisi kwa
kuwa jeshi hilo nalo linatuhumiwa.
No comments