Header Ads

Mbunge apewa mtihani wa uwekezaji


MBUNGE wa Shinyanga Mjini, Stephen Masele, amepewa mtihani wa uwekezaji viwanda mkoani hapa, kutokana na nafasi kubwa aliyoipata ya kuchaguliwa kuwa makamu wa Rais wa Bunge la Afrika.

Kutokana na nafasi hiyo, atakuwa na fursa ya kuzungumza na marais, watu mbalimbali na wafanyabiashara wakubwa na kuwashawishi kuja nchini kuwekeza katika viwanda.

Hayo yalisemwa juzi mjini Shinyanga kwenye mkutano wa hadhara na Mbunge wa Msalala wilayani Kahama, Ezekiel Maige, wakati akitambulisha wabunge walioambatana na Masele kwenda jimboni kwake kuwashukuru wananchi kwa kumchagua kuwa mbunge na pia kupata nafasi hiyo muhimu kwa Watanzania.

Maige alisema Mkoa wa Shinyanga una fursa nyingi za uwekezaji, lakini licha ya kuwa na rasilimali za kutosha, hauna viwanda ambavyo vya kutumia rasilimali hizo na kuupatia maendeleo, kuinua uchumi wa wananchi pamoja na vijana kupata ajira kwenye viwanda hivyo.

“Mbunge Masele kwa nafasi hiyo kubwa uliyoipata ya umakamu wa Rais wa Bunge la Afrika, tunatarajia mkoa wa Shinyanga utapata sasa kiwanda cha nyama, ngozi, maziwa, chuo cha madini, hospitali ya rufani,” alisema Maige na kuongeza kuwa Masele hanabudi pia kuupelekea mkoa huo teknolojia ya kilimo cha umwagiliaji.

“Naomba viongozi wa serikali mkoani Shinyanga muandike maandiko mbalimbali ya kuomba miradi zikiwamo fursa za uwekezaji kwa kuwa, kwa sasa tuna mtu ambaye atatusaidia kupata miradi hiyo kwa urahisi,” aliongeza Maige ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii.

Kwa upande wake, Masele alimtoa wasiwasi Maige na wananchi wa mkoa wa Shinyanga, kwa kueleza kuwa atahakikisha anatumia mbinu zote kuwashawishi wawekezaji kwenda Shinyanga na Tanzania kwa ujumla, ili nchi ipate kupiga hatua kimaendeleo kupitia uchumi wa viwanda.

Pia aliwaomba radhi wananchi wa jimbo la Shinyanga mjini kwa kutokuwapo jimboni humo kwa kipindi kirefu, kwa madai alikuwa akiitafuta nafasi hiyo muhimu ya umakamu wa Rais wa Bunge la Afrika, akisema  itakuwa chachu ya maendeleo kwa jimbo hilo na taifa kwa ujumla.



No comments

Powered by Blogger.