Watoto tisa waenda Israel kwaajili ya matibabu ya moyo
WATOTO tisa wa umri wa miezi tisa hadi miaka 14 waliozaliwa na matatizo ya moyo wameondoka jana kwenda nchini Israeli kwa ajili ya matibabu ya moyo.
Taarifa iliyotolewa jana na kitengo cha mawasiliano cha Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), imeeleza kuwa watoto hao wameambatana na wauguzi pamoja na wazazi wao.
Safari hiyo imeratibiwa na JKCI kwa kushirikiana na Taasisi ya Okoa Moyo wa Mtoto (Save a Child’s Heart – SACH) ya nchini humo.
“Taasisi yetu inatibu magonjwa mengi ya moyo (kwa asilimia 90) kwa watoto kupitia wataalamu wazalendo tulionao.
Hata hivyo, tunamkataba na Israel kwa baadhi ya wagonjwa wachache ambao ni asilimia 10 wanaohitaji utaalamu wa hali ya juu zaidi kuliko uliopo hapa nchini kwa sasa,” ilifafanua taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kuna ushirikiano mzuri na nchi ya Israel na Tanzania, na kwamba gharama za matibabu ya watoto hao zinagharamiwa na SACH.
Aidha, ilifafanua kuwa madaktari bingwa wa magonjwa ya moyo sita na wauguzi wanne wamesoma nchini Israel na hivi sasa wanatibu wagonjwa katika Taasisi hiyo.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa daktari mmoja na wauguzi wawili bado wanaendelea na masomo nchini humo, na kwamba itasaidia kwa siku za usoni zaidi ya asalimia 95 ya watoto watatibiwa hapa nchini.
Ilifafanua kuwa kundi hilo ni la sita la watoto kwenda kutibiwa magonjwa ya moyo nchini Israel tangu mwaka 2015 na Taasisi ya Moyo ilianza ushirikiano na Taasisi ya Okoa Moyo wa Mtoto wa kuwapeleka wagonjwa nchini humo.
Hadi sasa watoto 56 wameshatibiwa nchini humo na wanaendelea vizuri na kwamba wazazi na walezi wanatakiwa wasisahau kupima afya za watoto wao pale watakapoona kuna hali ya tofauti katika ukuaji wa mtoto kwa kuwa magonjwa mengi ya moyo yanaanzia utotoni.
“Mtoto akianza kuugua magonjwa ya moyo wazazi wengi wanadhani ni matatizo ya kifua baada ya kumfikisha mtoto hospitali na kufanyiwa vipimo ndipo inagundulikwa kuwa anasumbuliwa na magonjwa ya moyo,” ilifafanua taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa tarifa hiyo, wajawazito wameshauriwa wafanye uchunguzi (Fetal Echocardiography) wa kuangalia kama mtoto aliyeko tumboni ana matatizo ya moyo au la, na kwamba kupitia kipimo hicho mtoto akigundulika kuwa na tatizo la moyo atapatiwa matibabu kwa wakati na hivyo kuwa na afya njema kama watoto wengine.

No comments