Kufutwa kwa kesi ya Bemba kwazua ghadhabu
Gazeti la Süddeutsche lilikuwa na kichwa cha habari "Ghadhabu kuhusu Hukumu" Mahakama ya kimataifa ya uhalifu ya ICC mjini The Hague yamuachia huru makamu wa rais wa zamani wa Congo, Jean Pierre Bemba.
Mhariri wa gazeti la Süddeutsche Zeitung alisema wanaharakati wa kutetea haki za binadamu mwishoni mwa wiki iliyopita waliukosoa uamuzi wa mahakama ya ICC wa kumuondolea mashitaka mwanasiasa huyo wa Congo na kiongozi wa zamani wa waasi, Jean Pierre Bemba. Gazeti lilimnukuu msemaji wa shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International akisema hatua ya mahakama hiyo ni fedheha; ni kama kofi katika nyuso za wahanga. Naye Fiona McKay wa shirika la haki za binadamu la Open Society alinukuliwa akisema hatua hiyo ni pigo kubwa kwa mahakama ya ICC, ambayo kwa miaka kumi imetumia raslimali nyingi kushughulikia kesi ya Bemba. Bemba alihukumiwa kifungo cha miaka 18 jela katikati ya mwaka 2016 katika kesi ya kihistoria ambapo mbabe wa kivita aliwajibishwa kwa uhalifu ambao aliamuru au alioweza kuuzuia.
Nalo gazeti la Tageszeitung likizingatia pia hukumu hiyo, lilisema mbabe wa zamani wa kivita wa Congo, Jean Pierre Bemba, ameibua hisia mseto nchini mwake na miongoni mwa wanasheria katika ngazi ya kimataifa.
Mhariri anasema wafuasi wa Bemba nchini Congo wanamuona kama rais mtarajiwa. Haijawa wazi ikiwa Bemba atalazimika kukaa The Hague mwaka mwingine mmoja kwa kutiwa hatiani katika kesi nyingine ya kuwashawishi wapigaji kura, kwani tayari amekaa katika mahakama hiyo kwa miaka kumi.

No comments