Header Ads

Serikali yajipanga kukopa Trilioni 8.9


Katika mwaka wa fedha 2018/2019 Serikali imepanga kukopa jumla ya kiasi cha shilingi trilioni 8.9 kutoka soko la ndani na nje kwa masharti ya kibiashara, kwaajili ya kugharamia miradi ya maendeleo pamoja na kulipia dhamana za Serikali.

Kwa mujibu wa mapendekezo ya Serikali kuhusu mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2018/2019 iliyowasilishwa Bungeni na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango, Jijini Dodoma imeonesha Serikali itakopa trilioni 8.9 ambapo mkopo wa fedha za ndani utakua ni shilingi trilioni 5.7 na trilioni 3.1 ni mkopo kutoka fedha za nje.

“Serikali inatarajia kukopa shilingi trilioni 8.9 kutoka soko la ndani na nje kwa masharti ya kibiashara, mikopo ya ndani inatarajiwa kuwa shilingi trilioni 5.79 ambapo shilingi trilioni 4.6 kwaajili ya kulipia dhamana za Serikali zinazoiva, na shilingi trilioni 1.19 ni mikopo mipya kwaajili ya kugharamia miradi ya maendeleo ili kuongeza kasi katika ujenzi wa miundombinu serikali inatarajia kukopa shilingi trilioni 3.11 kutoka soko la nje” alisema Waziri Mpango.

Kwa upande mwingine serikali imepanga kukusanya jumla ya shilingi trilioni 20.8 kama mapato ya ndani, sawa na asilimia 64.3 ya bajeti, mapato hayo ni kutoka vyanzo vya Halmashauri, washirika wa maendeleo, mapato ya kodi na yasiyo ya kodi, mifuko ya pamoja ya kisekta na misaada ya kibajeti.

Katika mapendekezo ya serikali imepanga kukusanya na kutumia kiasi cha shilingi trilioni 32.4 katika mwaka wa fedha 2018/2019 na kati ya fedha hizo, shilingi trilioni 20.47 kwaajili ya matumizi ya kawaida na matumizi ya maendeleo yatakuwa shilingi trilioni 12.01 sawa na asilimia 37 ya bajeti.

No comments

Powered by Blogger.