Uhispania yawapokea wahamiaji waliokataliwa Italia na Malta
Bandari ya Valencia nchini Uhispania imepokea meli ya kwanza iliyokuwa imebeba wahamiaji waliookolewa kutoka kwenye bahari ya Mediterrania na kukataliwa kuingia Italia na Malta.
Meli tatu za kwanza ziliingia bandarini baada ya uda wa alfajiri.Baadhi ya wahamiaji kati ya 629 waliokolewa karibu na nchi ya Libya mwishoni mwa juma lililopita na meli ya Aquarius walianza kuingia.
Maafisa wa kitabibu na watafsiri wa lugha wamesema wako tayari kutoa usaidizi.
Serikali mpya ya kisoshalisti ya Uhispania imeahidi kuwapa huduma za afya bure na kuwa itafanyia uchunguzi kila anayeomba hifadhi.
''Ni jukumu letu kusaidia kuepuka majanga ya kibinaadamu na kutoa msaada wa kuwapatia mahali salama, tukifuata makubaliano ya kimataifa ya kuwa na jukumu la kulinda haki za binaadamu'', Waziri mkuu wa nchi hiyo,Pedro Sánchez alieleza mwanzoni mwa juma hili.
Meli ya doria ya Italia, iliingia kwenye bandari ya Valencia ikiwa na wahamiaji 274, Shirika la habari la Italia, Ansa liliripoti.
Meli ya pili , the Orione na nyingine ya Aquarius zimekuwa zikitarajiwa asubuhi ya jumapili zikiwa na wahamiaji waliobaki.
Maafisa wanasema wahamiaji waliookolewa wanahusisha watoto 11 chini ya umri wa miaka 13 na wanawake saba wajawazito.
Serikali ya Italia ilikataa meli ya Aquarius kutia nanga nchini humo, Waziri wake wa mambo ya ndani Matteo Salvini akisema kuwa si haki kubeba jukumu hilo , akitaka Malta ipokee wahamiaji hao, Malta nayo ikilikataa jukumu hilo.
Wafanyakazi wa shirika la msalaba mwekundu 1000 walikuwa tayari kuwapokea wahamiaji walipokuwa wakiteremka kutoka kwenye meli.Walikuwepo pia maafisa wa polisi kusaidia katika mapokezi hayo.

No comments