Ulinzi yaajiri maelfu ya vijana
BUNGE limeelezwa kuwa vijana 42,593 wameajiriwa na Vyombo vya ulinzi na usalama kuanzia mwaka 2003 hadi mwaka 2017.
Pia vijana 3,576 wameajiriwa na Suma Jkt Guard.
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Dk.Hussein Ali Mwinyi, aliyasema hayo jana alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Chumbuni (CCM) ,Ussi Salum Pondeza, ambaye alitaka kujua kuhusu vijana wa Kitanzania wanaokabiliwa na tatizo la ukosefu wa ajira, hivyo nguvu kazi kupotea badala ya kutumika kwa uzalishaji.
Dk. Mwinyi alisema idadi ya vijana walioajiriwa na vyombo vya ulinzi na usalama kuanzia mwaka 2003 hadi 2017 jumla yao ni 42,593 na idadi ya vijana 3,576 wameajiriwa na Suma JKT.
Alisema pamoja na mafunzo ya kijeshi ambayo vijana huyapata kwa muda wa miezi 6 vijana hao hujifunza shughuli mbalimbali za uzalishaji katika makambi wanayopangiwa baada ya mafunzo ya kijeshi.
Alisema shughuli hizo hufanyika ndani ya mwaka mmoja na nusu, kati ya miaka miwili ambayo wanajitolea wanapokuwa JKT.
“Baada ya kumaliza muda huo tunaamini vijana wanakuwa wamepata ujuzi ambao wanaweza kujiajiri au hata kuajiriwa,” alisema.
Alisema JKT lina mashamba makubwa ya kilimo yanayotumia pembejeo za zana za kilimo za kisasa za kilimo kama vile mbegu bora. Aidha alisema pamoja na mafunzo hayo vijana hupewa mafunzo ya ujasiriamali.

No comments