Mahakama ya Rufaa Tanzania imekubali maombi ya Bodi ya Wadhamini ya
Chama cha Wananchi (CUF) inayomuunga mkono Katibu Mkuu wa chama
hicho,Maalim Seif Sharif Hamad katika shauri Namba 43/01/2017 kuhusu
kumkataa Jaji Kihiyo kusikiliza shauri la msingi.
Taarifa hiyo ya maamuzi ya mahakama ya Rufaa, imetolewa mapema leo
Disemba 22, 2017 kwa vyombo vya habari na Naibu Mkurugenzi wa Habari
CUF, Mbarala Maharagande.
“Mahakama ya Rufaa imeipa ushindi Maombi ya Bodi ya Wadhamini ya CUF
chini ya Katibu Mkuu Maalim Seif Sharif Hamad katika shauri Namba
43/01/2017 (From Civil Application No.23/2017) kuhusu kumkataa Jaji
Kihiyo kusikiliza shauri la msingi tajwa hapo juu.
“Shauri hili ndilo linalohoji uhalali na mamlaka ya Msajili wa vyama vya
siasa nchini Jaji Francis Mutungi kumrejesha Lipumba katika nafasi ya
Uongozi ndani ya CUF baada ya kujiuzulu na kukubaliwa kujiuzulu kwake na
Mkutano Mkuu wa Taifa wa CUF uliofanyika katika ukumbi wa Blue Pearl,
Ubungo Plaza Tarehe 21 August, 2017,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, Jaji wa Mahakama ya Rufaa , Jaji Musa
Kipenka amekubaliana na hoja za Mawakili Wasomi wa CUF Halfani Daimu,
Juma Nassoro na Hashimu Mziray walizozitoa Mbele ya Mahakama hiyo.
Maharagande amesema, maamuzi hayo yanaipa nafasi mahakama kuu kuendelea
kusikiliza shauri hilo ambalo Msajili wa Mahakama Kuu ameshalipangia
jalada ambalo linasikilizwa mbele ya Jaji Wilfred Ndyansobera.
No comments