Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta na mwenzake wa Tanzania Dkt John Magufuli
wamekutana mjini Kampala, Uganda na kuahidi kuimarisha uhusiano kati ya
nchi hizo mbili.
Wawili hao wamewaagiza mawaziri wa nchi hizo mbili kutatua tofauti
ndogondogo zinazojitokeza katika biashara kati ya nchi hizi mbili.
Marais hao wametoa maagizo hayo walipokutana hoteli ya Munyonyo mjini
Kampala muda mfupi kabla ya kuanza kwa vikao vya mkutano wa wakuu wa
nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Uhusiano kati ya nchi hizo mbili ulikuwa umeonekana dorora wiki za
karibuni hasa kutokana na hatua ya Tanzania kuwakamata na kuwateketeza
vifaranga kutoka Kenya na pia kuwapiga mnada ng'ombe wa watu wa jamii ya
Wamaasai kutoka Kenya.
Wawili hao wamesema wanataka kuona biashara kati ya Tanzania na Kenya
inazidi kukua na bidhaa zinauzwa na kununuliwa baina ya nchi hizo bila
vikwazo vyovyote na hivyo kuagiza tofauti zilizojitokeza katika baadhi
ya bidhaa zimalizwe.
"Kuna mambo madogomadogo yanakuwa yanajitokeza katika biashara kati ya
Kenya na Tanzania, tunataka kwa haya yote Mawaziri wa Kenya na Mawaziri
wa Tanzania mkae myatatue, sisi hatuna tatizo, mambo mengine
madogomadogo mno, mambo ya viatu, nguo, ngano, gesi ni madogo sana,
mnatakiwa myatatue nyinyi yasifike kwetu, sisi huku tuko sawasawa"
amesema Dkt Magufuli, tamko ambalo limeungwa mkono na Bw Kenya.
Wametoa maagizo hayo kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki wa Tanzania Dkt. Augustine Mahiga, Waziri wa Katiba na Sheria
wa Tanzania Prof. Palamagamba Kabudi upande wa Tanzania.
Upande wa Kenya, maagizo yametolewa kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya
Balozi Monica Juma na Waziri wa Afrika Mashariki na Maendeleo ya
Ushoroba wa Kaskazini wa Kenya Peter Munya.
No comments