Ripoti ya uchunguzi wa kifo cha mwanafunzi aliyepigwa risasi na polisi yazua tafrani muhimbili
Ndugu wa mwanafunzi wa Chuo cha Taifa
cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwiline aliyeuawa kwa kupigwa risasi
na polisi, jana walisusia kwa muda kuchukua mwili wa binti huyo
wakishinikiza Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kueleza sababu za kifo
chake.
Jambo hilo lilizua sintofahamu kabla ya kutulizwa kwa kuelezwa kwa mdomo na madaktari kuwa alipigwa risasi kichwani.
Jana asubuhi, ndugu hao walikusanyika
katika eneo la chumba cha kuhifadhia maiti Muhimbili wakisubiri
uchunguzi ukamilike ili kujua hatima ya kuusafirisha mwili kwa ajili ya
mazishi yatakayofanyika wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro Ijumaa baada
ya mwili huo kuagwa Alhamisi katika viwanja vya NIT, Mabibo.
Wakati wakiendelea kuvuta subira
walielezwa na madaktari waliochunguza mwili huo kuwa ripoti ya uchunguzi
itatolewa baada ya siku 14 jambo ambalo hawakukubaliana nalo, huku dada
wa mwanafunzi huo, Tegolena Uiso akisema hawatapokea mwili bila
kuelezwa nini kilichomuua ndugu yao.
“Sisi tumekuja kwa ajili ya kujua hasa
ndugu yetu nini kimemkuta hatuwezi kupokea mwili bila ripoti.
Wanatuambia ni baada ya wiki mbili sina hakika kama hawajabaini kitu
chochote, hatuwezi kuuchukua mwili mpaka tupewe sababu,” alisema
Tegolena.
Tegolena alisema walizungumza na Mkuu wa
Chuo cha NIT, Profesa Zakaria Mganilwa aliyekuwa akiwasiliana na
madaktari hao, mpaka saa saba mchana hawakuwa na majibu yoyote.
Awali, Profesa Mganilwa alisema wamefika hospitalini hapo kufuatilia uchunguzi huo akiwa na ndugu wa marehemu.
Akwilina alikuwa mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Shahada ya Ununuzi wa Ugavi katika chuo hicho.
Alipigwa risasi Februari 16 eneo la
Mkwajuni, Kinondoni wakati polisi wakiwatawanya wafuasi wa Chadema
wakiongozwa na mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe waliokuwa
wakielekea katika ofisi ya msimamizi wa uchaguzi Jimbo la Kinondoni,
Aron Kagurumjuli kudai hati ya viapo vya mawakala.
Mwili wake ulihifadhiwa katika Hospitali
ya Mwananyamala kabla ya kuhamishiwa Muhimbili kwa ajili ya kufanyiwa
uchunguzi ambao ndugu hao walifika jana hospitali hapo ili kujua sababu
ya kifo chake.
Mwananchi lilishuhudia ndugu wa Akwilina
wakiwa wamesimama kwa vikundi nje ya chumba hicho cha kuhifadhia maiti,
na ilipofika saa nane mchana, Profesa Mganilwa alionekana kuzungumza na
madaktari na baadaye kuwaeleza ndugu hao majibu ya uchunguzi.
Akizungumza na Mwananchi kuhusu
walichoelezwa, shemeji wa mwanafunzi huyo, Festo Kavishe alisema
uchunguzi umeonyesha Akwilina alijeruhiwa vibaya kichwani.
“Ripoti ambayo tumepewa imeonyesha
kwamba kichwa cha marehemu kilipasuliwa vibaya na risasi ambayo
iliingilia upande wa kushoto kwa kichwa chake na kutokea upande wa kulia
ambao umefumuka vibaya,” alisema.
Alisema wameridhishwa na sehemu ya
ripoti ya uchunguzi huo na sasa wanakwenda kufanya kikao cha ndugu
kujadili namna gani watampumzisha Akwilina.
Alisema iwapo madaktari wasingewapatia
majibu hayo, wasingethubutu kuuchukua mwili huo kwa mazishi, kwa sababu
walihitaji kupata picha kamili ya nini kilimuua Akwilina.
“Sasa tumeshafahamu nini kimemuua ndugu
yetu kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na madaktari baada ya uchunguzi,
hivi sasa tunakwenda kujadiliana kuhusu mazishi yake,” alisema Kavishe
jana.
Mazishi ya Akwilina
Baada ya kutoka Muhimbili, ndugu hao
walifanya kikao cha kupanga shughuli ya mazishi na baadaye kaka wa
marehemu, Moi Kiyeyeu kueleza kuwa Akwilina atazikwa Ijumaa. “Tutamuaga
ndugu yetu siku ya Alhamisi katika viwanja vya chuo cha NIT pale Mabibo
na siku hiyohiyo tutaanza safari kuelekea Rombo-Mashati Olele mkoani
Kilimanjaro na mazishi tutafanya Ijumaa,” alisema Kiyeyeu.
Baba atamani kumkabili muuaji
Akwiline Shirima, ambaye ni baba mzazi
wa Akwilina katika mahojiano na Mwananchi jana alisema siku akikutana na
polisi aliyemuua mwanae, atapambana naye.
Wakati baba akiapa kupambana na muuaji
wa mwanae kama atakutana naye, Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini aliomba
kuundwa tume huru kuchunguza mauaji hayo.
Akizungumza nyumbani kwake Kijiji cha
Olele jana, Shirima alisema endapo muuaji atakuwa ni kijana mwenye nguvu
kumzidi, atapambana naye hata kwa kumuuma kwa meno.
“Najua ni ngumu kukutana na aliyempiga
mwanangu risasi, lakini laiti ningekutana naye kama ni kijana mwenye
nguvu kunizidi ningepambana naye hata kumuuma kwa meno,” alisema.
“Na kama ni mzee mwenzangu ningepambana
naye hadi kifo ila kwa bahati mbaya siwezi kumpata hivyo sina namna. Kwa
kweli hiki kifo kimezima ndoto ya familia ya kuondokana na umaskini.”
Shirima aliiomba Serikali kuliangalia
suala hilo kwa kina na kuona namna ya kumsaidia kwa kuwa tegemeo lake
limeondoka na wao kwa sasa hawana msaada wowote na wanachosubiria ni
kifo.
“Jamani hii ni taa yangu imezimika na
kuniacha gizani kwani tangu nimepata taarifa za kifo chake sijaweza kula
chochote. Nimekuwa kama nguruwe aliyetelekezwa porini bila msaada,”
alisema Shirima.
“Nilipopata taarifa za kifo cha mwanangu
nilishtuka sana, na kuhoji ni mwizi au nini kimetokea, lakini baadaye
nikaambiwa ni polisi imefanya mambo hayo. Imenitia uchungu sana na
siwezi hata kula.”
Shirima alisema afadhali mwanaye
angekuwa mgonjwa akamuuguza kuliko kifo cha ghafla alichokipata ambacho
kimewaacha kwenye hali ambayo haitafutika mioyoni mwao katika maisha yao
yote.
Mama wa marehemu, Costanzia Akwiline
alisema mauaji ya mwanaye ni ya kinyama na bora angekuwa mbuzi angekula
nyama kujifariji kuliko kwa mwanaye ambaye hakuna anayeweza kumfuta
machozi.
“Mwanangu hakuwa mwanasiasa, aliuawa
akiwa kwenye gari akielekea kwenye shughuli zake, familia tulijinyima
tukajichanga kwa kushirikiana na majirani ili asome aje atokomboe,”
alisema.
“Lakini leo nasubiria niletewe maiti
kwenye jeneza. Kwa kweli imeniuma sana na kunikatisha tamaa. Naomba
Serikali itende haki katika tukio hili.”
Romana Akwiline, ambaye ni dada wa
marehemu aliiomba Serikali kusaidia jambo hilo na kuhakikisha
waliohusika na mauaji hayo aliyosema ni ya kinyama wanachukuliwa hatua
ili liwe fundisho.
Akizungumzia maisha ya Akwilina, alisema
baada ya mdogo wao kuonekana anapenda elimu, ndugu walijichanga kwa
kushirikiana na majirani ili kuhakikisha anatimiza ndoto zake.
“Familia yetu kama mnavyoiona ni watu
maskini. Wazazi wetu ni wakulima na sisi ndugu zake tumeishia darasa la
saba, huyu tulidhani ndiye atakuja kuwa mkombozi wa familia,” alisema.
Alisema pamoja na matumaini hayo makubwa
ya familia, hawakujua kuwa yalikuwa ni mawazo yao tu ambayo yasingeweza
kutimia kutokana na mtu mmoja kuchukua uhai wake.
Alisema katika familia yao wako wanane
na mtoto mwingine ambaye anasoma yupo kidato cha tatu na kwamba kutokana
na tukio hilo wanaweza kukata tamaa ya kumsomesha.
“Tulitegemea marehemu anaweza kuja
kumsaidia mdogo wake huko mbeleni ili naye afike chuo kikuu na
kushirikiana kuikomboa familia. Hili linaweza kuwavunja moyo
wanaojitolea,” alisema.
Mwanaukoo Dismas Shirima alisema
marehemu alikuwa na uchungu wa maisha licha ya umri wake kuwa mdogo,
hali iliyomsukuma kujituma kusoma kwa bidii ili kuinua familia yake.
“Kutokana na upeo wake na mtazamo wa
kuona mbali, alijituma katika kusoma na hii iliwafanya watu wengi kutoa
misaada ili apate elimu kumwezesha kutimiza ndoto zake,” alisema.
Shirima alisema ni vyema jamii ikatambua kuwa hakuna aliyepanga Akwilina auawe na waepuke kuingiza siasa katika jambo hilo.
Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Grace
Kiwelu alisema kifo cha Akwilina kimeleta masikitiko katika jamii, hasa
familia yake ambayo iliweka matarajio makubwa kwake.
Polisi watoa neno uchunguzi
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es
Salaam, Lazaro Mambosasa alipoulizwa kuhusu uchunguzi wa tukio hilo
alisema polisi haiwezi kutoa taarifa wakati uchunguzi unaendelea.
“Uchunguzi unapofanyika hatuwezi kuwajulisha tukimaliza tutaeleza nani amekamatwa kwa hiyo tupeni nafasi tufanye kazi,” alisema.
Imeandikwa na Herieth Makwetta, Elizabeth Edward na Mwafatma Hamis (Dar), Florah Temba na Janeth Joseph (Moshi).

No comments