Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi Mwanasheria wa
Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza, Alphonce Sebukoto
kupisha uchunguzi wa tuhuma za kuharakisha malipo ya fidia ya Sh279
milioni inayomilikiwa na kampuni ya mwenyekiti wa halmashauri hiyo,
Anthony Bahebe.
Majaliwa ambaye yuko kwenye ziara ya siku saba mkoani Mwanza amechukua
uamuzi huo leo Februari 19 alipokuwa akizungumza na watendaji na
watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Misungwi.
Kabla ya kuwa diwani na kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa halmashauri,
Bahebe alikuwa akitekeleza mradi wa maji katika halmashauri hiyo wenye
thamani ya zaidi ya Sh300 milioni kupitia kampuni yake ya Seekevim
Company Ltd ambayo iliishtaki halmashauri.
“Wewe mwanahseria uliyeajiriwa kwa kazi ya kuitetea halmashauri
hukutimiza wajibu wako katika shauri hili kwa sababu licha ya kusema
mahakamani kuwa halmashauri haina pingamizi na madai hayo, pia
uliharakisha malipo ya fedha hizo ulipokaimu nafasi ya mkurugenzi,”
amesema
Majaliwa na kuongeza:
"Utasimama kazi kuanzia leo kupisha uchunguzi na ikibainika kweli
hukutekeleza ipasavyo majukumu yako, basi utumishi wako utaishia hapo
hapo maana Serikali haiwezi kuvumilia kuendelea kuwa na watumishi wa
aina hii.”
Waziri Mkuu ameonyesha mshangao kwa mwenyekiti wa halmashauri kuishtaki
na kuidai fidia halmashauri anayoiongoza hadi kuchukua mamilioni ya
fedha ambazo zingetumika kutekeleza miradi ya maendeleo.
“Hata kama shauri hili lilifunguliwa kabla hajagombea udiwani na kuwa
mwenyekiti; baada ya kushika wadhifa huu angetafuta utaratibu mwingine
wa kulimaliza suala hili,” amesema Waziri Mkuu.
Amesema uchunguzi wa awali umebaini fedha hizo zimelipwa haraka haraka
kupitia akaunti binafsi kwenye moja ya matawi ya benki jijini Mwanza.
Ziara hiyo pia haijamwacha salama Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri
hiyo, Eliud Mwaiteleke baada Waziri Mkuu kutangaza kutuma timu maalum ya
uchunguzi dhidi ya tuhuma za upotevu wa mamilioni ya fedha zilizotumwa
kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo.
“Halmashauri ilipata Sh548 milion kutoka Serikali Kuu kwa ajili ya
ujenzi wa daraja lakini zaidi ya Sh50 milioni hazijulikani zimefanya
nini,” amesema Majaliwa.
Ametaja fedha nyingine ambazo hazijulikani zilipo na zitakazochunguzwa
kuwa ni Sh325 milioni ambazo ni kati ya Sh665 milioni zilizotumwa kwa
ajili ya miradi ya Rivemp unaosaidia uhifadhi wa mazingira katika maeneo
ya Bonde la Ziwa Victoria.
"Nitaleta watu kuchunguza fedha hizi ambazo zinadaiwa kubadilishiwa
matumizi badala ya kutekeleza miradi iliyokusudiwa,” amesema Waziri Mkuu
No comments