Hatimaye yule mtanzania aliyesaidiwa kupata ufadhili wa matibabu na
Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam, Mhe Paul Makonda amewasili leo hii majira
ya saa 9:20 alasiri katika Uwanja wa kimataifa wa Beijing Capital.
Mtanzania huyo aitwaye Ahmed Albaity alipokekewa na Maafisa waandamizi
wa ubalozi pamoja na watanzania waishio hapa jijini Beijing na
kusindikizwa kwenye hospitali ya kimataifa ya Puhua.
Ndugu Ahmed Albaity ambaye amekuwa akisumbuliwa na tatizo la uti wa
mgongo ambalo limedumu kwa takribani miaka kumi na moja akiwa
kitandani,tayari ameanza kupatiwa Matibabu katika hatua za awali
mara tu baada ya kuwasili hospitalini hapo.
Mapema akizungumza kwa niaba ya Wanafunzi wakitanzania Wanaosoma na
kuishi nchini humo Bw. Remidius Emmanuel ambaye pia ni Katibu Mkuu
Shirikisho hilo amesema wao kama watanzania wanaosoma na kuishi katika
Taifa la China wameshiriki kumpokea Mtanzania mwenzao (Ndugu. Ahmed
Albaity ) na kwamba kwa kipindi chote ambacho atakuwepo hapa Beijing
China wataendelea kutoa Ushirikiano na kumjulia hali wakati wote.
"Tunamshukuru Mwenyezi MUNGU amemuongoza Bw.Ahmed kufika salama hapa
Beijing, Tumeshuhudia watanzania wakimsindikiza uwanja wa ndege wa
Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam na kuongozwa na Mkuu wa
Mkoa wa Dar es Salaam Mhe.Paul Makonda, huu ni upendo wa kipekee, na
sisi tumeguswa na kuwiwa kumpokea tukiongozwa na Maafisa waandamizi wa
Ubalozi wetu hapa China" Alisema Bw. Remidius.
Kwa upande wake ndugu Ahmed Albaity ameushukuru Ubalozi wa Tanzania
nchini China pamoja na uwakilishi wa Watanzania wanaosoma na kuishi
nchini humo kwa moyo wao wa upendo na namna walivyoweza kumpokea yeye na
ujumbe alioambatana nao.
Bw.Michael Semindu moja kati watanzania wanaosoma nchini humo
aliyeshiriki mapokezi hayo alimhakikishia Ndugu Ahmed Ushirikiano kwa
kipindi chote atakachokuwa kwenye matibabu jijini Beijing "Nimefurahi
kuungana na Maafisa wa Ubalozi pamoja na watanzania wenzangu kumpokea
mwenzetu, tunamuahidi ushirikiano kwa kipindi chote atakachoendelea
kupata matibabu nchini China" Alisema Bw. Michael
No comments