Kilimo cha bora cha mpunga
Mpunga
ni zao la pili la chakula kwa umuhimu linalolimwa sehemu nyingi nchini
Tanzania. Umuhimu wa zao hili umeongezeka kuanzia muongo uliopita
kutokana na jamii za mijini na vijijini kupendelea zaidi kula wali na
kupunguza ulaji wa vyakula vingine na kulifanya zao hili kuwa la chakula
na biashara.
Mvua
ni chanzo kikuu cha maji kwenye kilimo cha mpunga. Viwango vya mahitaji
ya maji katika kukua kwa mpunga hutofautiana miongoni mwa aina za
mpunga. Ni kwa jinsi hii mpunga hupandwa katika mazingira mbalimbali
kutegemea na mahitaji yake ya maji. Zipo aina tatu kuu za mazingira
yanayolimwa mpunga kulingana na upatikanaji wa maji na hali ya mwinuko
wa nchi. Mazingira haya ni kilimo cha mpunga wa mabondeni kinachotegemea
mvua (72%), kilimo cha mpunga wa kwenye miinuko (20%) na kilimo cha
mpunga cha umwagiliaji (8%).
Kiasi
cha mpunga kinachozalishwa nchini kimekuwa kikiongezeka mwaka hadi
mwaka kutoka tani 41,000 mwaka 1970 hadi tani 811,500 mwaka 1998.
Ongezeko hili limetokana na kuongezeka kwa eneo linalolimwa mpunga na
kwa kiasi kutokana na kuongezeka kwa miradi midogo ya umwagiliaji pamoja
na matumizi ya tekinolojia bora za kilimo.
Maeneo
yanayolima mpunga kwa wingi Tanzania: ni Morogoro maeneo ya bonde la
kilombero/Ifakara, Dakawa, Malolo; Mbeya: Kyela, Mbarali; Shinyanga:
Kahama; Mwanza, Bonde la Ruvu mkoani Pwani. Na maeneo mengine mengi.
![]() |
| Shamba la mpunga |
pH ya udongo (Soil pH)
pH
ni kipimo kinachoonyesha kiwango cha tindikali au nyongo katika udongo.
Udongo waweza kuwa tindikali (ph ndogo kuliko 7), nyongo (ph kubwa
kuliko 7), au katikati (neutral) – ph ya 7. Tindikali au nyongo ya
udongo hupimwa kwa kutumia pH mita. Mazao mengi hustawi zaidi katika
udongo wenye hali ya tindikali ya wastani (kipimo cha pH 5.5 hadi 7.0).
Mpunga hustawi kwenye udongo wa mfinyanzi wenye tindikali ya wastani na
virutubisho vya kutosha.
Kuandaa Shamba, Kupanda na Kupalilia
Kuandaa shamba, kusafisha, kulima/kutifua
Ni
vyema mashamba yaandaliwe mapema kabla ya msimu wa kupanda haujaanza
ili kumpa mkulima fursa ya kupanda kwa wakati unaotakiwa. Kuna njia
mbalimbali zinazotumika kuandaa mashamba. Kati ya njia hizi ni pamoja na
kufyeka, kung’oa visiki na kulima. Shamba linaweza kulimwa kwa kutumia:
- Jembe la mkono – wengi wanatumia
- Jembe la kukokotwa na wanyama kama ng’ombe
- Power tillers
- Matrekta
Baaada
ya kulima, shamba linawekwa maji ili liloane vizuri na kisha udongo
unachanganywa vizuri na maji ili kutengeneza tope. Hii ni kuchavanga
(puddling). Hii inarahisisha:
- Kupandikiza miche
- Kuhifadhi maji
Mbegu Bora za Mpunga
Matumizi ya mbegu bora ni muhimu katika upatikanaji wa mavuno mengi na bora. Kuna makundi mawili makuu ya mbegu ambayo ni:
Mbegu za asili za mpunga:
Ni zile ambazo zimetumika miaka mingi katika historia ya kilimo. Kuna
aina nyingi za mipunga ya asili inayolimwa sehemu mbalimbali hapa nchini
kama Supa, Kahogo, Kula na Bwana, Shingo ya mwali, n.k. Wakulima
wanazipenda mbegu hizi kutokana na kuwa na sifa kama vile ladha nzuri,
uvumilivu wa matatizo mbalimbali ya kimazingira na kwa sababu ya uwezo
wa mbegu hizi kustahimili katika hali mbaya ya hewa na hazihitaji
uangalizi wa hali ya juu.
Sifa
hizi ni matokeo ya mbegu hizi kumudu mazingira na uchaguzi wa mbegu
uliofanywa na wakulima kwa miaka mingi. Hata hivyo, nyingi ya mbegu hizi
zina uwezo mdogo wa kuzaa, zinachelewa kukomaa, ni ndefu na rahisi
kuanguka.
Mbegu zilizoboreshwa:
Hizi ni zile zilizoboreshwa kutokana na mbegu za asili. Mfano wa mbegu
zilizoboreshwa ni kama vile Katrin, IR54, na IR64. Zinazaa sana hasa kwa
kilimo cha umwagiliaji. Hata hivyo, hazikidhi ladha ya walaji na
ukobolekaji wake si mzuri na baadhi hazistahimili kwenye mazingira mengi
ya kawaida. Hii imezifanya mbegu hizi kukubalika na wakulima kwa
kiwango kidogo sana.
Mbegu
bora nyingine zilizozalishwa kutoka utafiti na kuonekana kupendwa kwa
ajili ya mavuno mengi na ladha nzuri kama TXD88 na TXD85. Hivi karibuni
imetolewa mbegu nyingine iitwayo TXD306 (SARO5), mbegu hii hupendwa na
wakulima, wafanyabiashara na walaji kutokana na sifa yake ya mavuno
mengi, punje ndefu kiasi na nzito, ladha nzuri na yenye kunukia pindi
ipikwapo na kuliwa.
Mbolea za kupandia mpunga
Kabla
ya kuweka mbolea hakakisha kuwa majaruba yanatengenezwa ili kuhakikisha
maji hayaingii na kutoka kiholela. Mbolea ya kupandia huwekwa kwa kusia
katika jaruba kabla ya kuchavanga. Kuchavanga husaidia kuchanganya
udongo na mbolea na pia kutengeneza eneo zuri la kupandikiza miche.
Baadaye miche hupandikizwa.
Viwango vya mbolea za kupandia mpunga
Kiwango
cha mbolea za kupandia kilichopendekezwa ni kilo 20 phosphate (P) kwa
hektari ambayo ni sawasawa na kiasi mifuko mitatu kwa hekta ya DAP (=
mfuko mmoja kwa ekari), au mifuko miwili kwa hekta ya Minjingu Phosphate
(= mfuko mmoja na nusu kwa ekari) au mifuko minne na nusu kwa hekta ya
Minjingu Mazao (= mifuko miwili kwa ekari).
Jinsi ya kupanda mpunga Kitaalam
Kuna
njia mbili kuu zinazotumika kupanda mpunga shambani. Njia hizo ni ile
ya kupanda mbegu moja kwa moja shambani na ile ya kupandikiza miche.
- Kupanda mbegu moja kwa moja
Njia
hii hutumika kwa kupanda mbegu moja kwa moja kwenye shamba
lililotayarishwa vizuri. Njia ya kawaida waitumiayo wakulima ni ile ya
kumwaga na kufukia mbegu (broadcasting). Njia zingine ni zile za kupanda
mbegu kwenye mashimo yaliyo kwenye mstari na kwa kuzingatia nafasi
maalum au mbegu hupandwa kwenye mashimo bila kufuata mstari na bila
kuzingatia nafasi iliyopendekezwa (dibbling). Vile vile mbegu hupandwa
kwa kunyunyizwa kwenye vifereji vyenye vina vifupi na kufukiwa pasipo
kuwa na nafasi kati maalum kati ya punje na punje (seed drilling)
- Kupandikiza miche
Njia
hii hutumika kwa kupanda mbegu kwanza kwenye kitalu kabla ya
kuzihamishia shambani. Mara nyingi mbegu zetu hutumia wiki tatu hadi nne
baada ya kuota kwenye kitalu na kufikia umri wa kupandikizwa shambani.
Katika shamba la mpunga miche hupandikizwa shambani kwenye mstari na kwa
nafasi maalum au kupandikizwa holela bila kuzingatia nafasi maalum za
kupanda.
Inashauriwa
kupandikiza miche katika kina cha sentimeta 2 hadi 3. Ukipanda kina
kirefu machipukizi huchelewa kujitokeza. Baada ya kupandikiza miche,
machipukizi hujitokeza baada ya siku 5 hadi 10.
![]() |
| Kupandikiza miche ya mpunga |
Nafasi ya kupanda mpunga
Nafasi
ya kupanda mpunga mbegu bora ni sm 15 kwa sm 15 au sm 20 kwa sm 20.
Kwenye mpangilio wa mistari miwili miwili (double rows), nafasi kati ya
mistari miwili ni sm 10, nafasi kati ya mmea na mmea katika kila mstari
ni sm 20, na nafasi kati ya mistari miwili na mistari miwili mingine
(double rows) ni sm 40. Mbegu za asili zipandwe kwa nafasi ya sm 20 kwa
sm 20 au sm 25 kwa sm 25 au sm 30 kwa sm 30.
Kupanda
kwa nafasi ni kati ya njia bora za kilimo inayomwezesha mkulima kupata
mazao bora. Hivyo ni muhimu sana kuzingatia kupanda kwa mistari na
kufuata nafasi zinazoshauriwa na wataalamu wa kilimo.
Muda wa kupanda
Muda
wa kupanda unatofautiana kutoka eneo moja kwenda jingine kulingana na
majira ya mvua. Kwa mfano katika wilaya ya Morogoro tarehe za kupanda ni
kuanzia desemba hadi januari kwa mpunga wa muda mrefu. Kwa mpunga wa
muda wa kati na muda mfupi, tarehe ya kupanda ni februari hadi machi.
Kupalilia Mpunga
Ni
muhimu shamba lipaliliwe ili kuondoa magugu. Magugu ni mimea hivyo
hushindana na mimea iliyopandwa na mkulima kwa kunyonya virutubisho
ardhini. Magugu yanaweza pia kuhifadhi wadudu na magonjwa yanayoweza
kushambulia mimea iliyopandwa na hivyo kupunguza mavuno.
Katika
kilimo cha mpunga, ni muhimu shamba lipaliliwe siku 14 hadi 21 baada ya
mimea kuota kufuatana na hali ya shamba wakati wa kupanda. Ni vizuri
katika kilimo cha mpunga, shamba lipaliliwe mara mbili, kutegemeana na
hali ya magugu katika shamba. Unaweza kupalilia kwa kung’olea kwa mkono,
kwa mashine au kwa kutumua viua magugu (herbicides) kama vile 2, 4-D
(Two Four D).
Utafiti
unaonyesha kwamba, shamba la mpunga ambalo halijapaliliwa linaweza
kupunguza mavuno kwa asilimia 60 hadi 100 ya mavuno yanayotarajiwa. Hata
kama mkulima atatumia mbegu bora, aina na kiasi cha mbolea
zinazoshauriwa, kupanda kwa mstari pamoja na mbinu nyingine bora
zinazoshauriwa, bila kupalilia hali hii itaathiri mavuno yake.
Mbolea za kukuzia mpunga
Ni
mbolea zinazotumika baada ya mimea kuota kwa lengo la kuikuza mimea ili
itoe mavuno bora. Mara nyingi mbolea hizi zinatoa kirutubisho cha
naitrojeni. Kiwango
kinachopendekezwa ni kilo 60 naitrogeni kwa hektari, ambacho ni
sawasawa na kiasi cha mifuko miwili ya UREA au Minne na Nusu Ya CAN au
Mitatu ya SA. Mbolea inayotumika mara kwa mara ni Urea. Hata hivyo
mbolea zingine kama SA inaweza kutumika kama kuna mahitaji ya salfa. CAN
inaweza kutumika kama kuna mahitaji maalum ya nitrate na ammonium.
Kwenye mpunga, mbolea ya kukuzia inawekwa wiki mbili baada ya
kupandikiza miche na irudie tena baada ya wiki nne.
Kuweka mbolea:
Mbolea ya kukuzia hutiwa kwa kusia wiki mbili baada ya kupandikiza, na
kurudia mwezi mmoja baadaye. Ni vyema kuweka mbolea za kukuzia mara
mbili ya kiasi kinachopendekezwa.
![]() |
| Shamba la mpunga uliopandwa kwa mistari |
Kudhibiti Magonjwa na Wadudu Wanaoshambulia Mpunga
Magonjwa Yanayoshambulia Mpunga
Magonjwa ya mpunga yamegawanyika katika makundi matatu kulingana na vimelea visababishi ambavyo ni fungasi, virusi na bakteria.
i) Rice blast (Ukungu)
Unaosababishwa na Pyricularia oryzae.
Dawa/Kudhibiti:
Mbegu bora inayostahimili ugonjwa, kupanda mapema, kung’oa mimea
iliyoathirika ama kunyunyiza dawa za kuua ‘vectors’ kama vile inzi weupe
(white flies).
ii) Brown leaf spot
Unaosababishwa na Helminthosporium spp.
Dawa/Kudhibiti: Panda mbegu kwa udongo unaofaa, weka mbolea ya kuzuia au tibu mbegu na dawa.
iii) Sheath rot
Unaosababishwa na Acrocylindrium oryzae.
Dawa/Kudhibiti: Kwa sasa hakuna njia ya kuzuia
iv) Rice Yellow Mottle Virus (RYMV) – Kimnyanga
Hivi karibuni ugonjwa wa kimyanga umetajwa kama ugonjwa hatari sana kwa mpunga hapa Tanzania.
Dawa/Kudhibiti: Panda mbegu zilizoboreshwa, zinazostahimili magonjwa au ng’oa mimea iliyoathirika.
Magonjwa
yasababishwayo na bakteria nayo wametajwa kuwa na madhara makubwa kwa
uzalishaji wa mpunga hapa nchini. Bakteria hawa wanajumuisha Acidovorax
avenae subsp. Avenae asababishae ugonjwa wa bacterial stripe, Pantoea
aglomerans, asababishae ugonjwa wa palea browning na Xanthomonas oryzae
p.v. oryzae.
Wadudu wanaoshambulia mpunga
Kuna
aina nyingi sana za wadudu wanaoathiri mpunga katika hatua mbalimbali
za ukuaji wa mpunga. Wanapokithiri na wasipodhibitiwa hupunguza kiasi
cha mavuno shambani.
i) White flies (Funza weupe)
Dawa/Kudhibiti: Nyunyiza dawa ya Thiodan, Endosulfan (Thionex), Fipronil (k.m. Regent 3G), Fenthion (k.m. Lebaycid)
ii) Rice stalk borer waharibifu
Kudhibiti:
Nyunyiza dawa ya Thiodan, Endosulfan (Thionex), Fipronil (k.m. Regent
3G), Fenthion (k.m. Lebaycid) Ili mkulima aweze kupata mazao mengi na
bora inashauriwa kutumia dawa za kuzuia magonjwa na wadudu
wanaoshambulia mimea na njia zinginezo.
Kuvuna, Kukausha, Kusafisha na Kuhifadhi
Kuvuna:
Mpunga uko tayari kuvuna wakati asilimia themanini (80%) ya rangi ya
mpunga kwenye masuke imebadilika na kuwa dhahabu. Mpunga unavunwa kwa
kukata bua pamoja na suke lake.
![]() |
| Uvunaji wa mpunga |
Kukausha:
Rundika pahali pakavu k.m. kwenye tuta la jaruba halafu pigapiga
(thresh) ili kutenganisha masuke na mpunga. Kama mpunga hayajakauka
vizuri hukaushwa zaidi juani kwa siku 3-4 ili kupunguza unyevunyevu
kufikia kiwango kinachofaa kwa kuhifadhi (14%). Ni muhimu mpunga ukauke
vizuri ili usioze ukiwekwa ghalani.
Kusafisha: Mpunga uliyokauka vizuri hupepetwa na vilevile mapepe huondolewa.
Kuhifadhi: Mpunga safi huwekwa kwenye gunia na magunia kupangwa vizuri ghalani juu ya mbao yasiguse sakafu.




No comments