Mamlaka ya usimamizi wa Bima nchini (TIRA) imetoa onyo kali kwa watu
wanaowatapeli wananchi kwa kuwauzia bima za kugushi na hivyo
kuwasababishia hasara na kuikosesha Serikali mapato,Matapeli hao ambao
wengi wao hawana leseni za kufanya biashara ya Bima wametakiwa kuacha
mara moja wizi huo kwani mkono wa sheria unawasaka ili hatua za kisheria
ziweze kuchukuliwa dhidi yao.
Akizungumza wakati wa zoezi la ukaguzi wa bima katika Vyombo vya moto
lililofanyika Mjini Dodoma ,Bibi Stella Guli Rutaguza amesema jumla ya
magari 586 yalifanyiwa ukaguzi, ambapo wamebaini magari 25, pikipiki
za miguu mitatu 5(bajaj) pikipiki za miguu miwili 2 yakiwa na Bima za
kugushi huku magari mengine 19 yakiwa hayana bima.
Rutaguza amesema kuwa wamefaminikiwa kuwakamata watu Wawili ambao
wanatuhumiwa kujihusisha na kuuza bima za kugushi kwa wananchi na tayari
wako mikononi mwa Jeshi la Polisi kwa hatua zaidi za kisheria.
Bibi Stella Rutaguza amesema zoezi la kuwasaka watu wanaouza bima feki
kwa na kuwaibia wananchi na Serikali ni endelevu hapa Dodoma na Nchi
nzima kwa ujumla.
"Tunataka kukomesha tabia hii chafu kwenye Soko la Bima", hivyo
tunawataka vishoka wa Bima popote walipo watafute kazi halali ya kufanya
maana Mamlaka ya Usimamizi wa Bima haitawafumbia macho na mkono wa
sheria hawataukwepa", alisema Rutaguza.
Amewataka wananchi kuchukua tahadhari ya kutokuibiwa na matapeli hawa wa
Bima kwa kununua Bima kwenye ofisi zilizosajiliwa na kupewa Leseni na
Serikali kwa ajili ya kufanya biashara ya Bima na kuacha kununua Bima
kiholela mitaani kwa watu wasiofahamika.
No comments