Kiongozi wa Upinzani afutiwa hati ya kusafiria
Serikali nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC, imeifuta hati ya kusafiria ya Kiongozi wa upinzani, Moise Katumbi, baada ya maelfu ya wafuasi wake kukusanyika katika mkutano Jijini Kinshasa.
Ofisi ya Katumbi ilibaini kufutwa kwa hati yake ya kusafiria siku ya Jumatano wakati akikamilisha taratibu za kuingia nchini Ubelgiji akitokea nchini Israeli
Serikali ya DRC kupitia Msemaji Wake, Lambert Mende, inadai hati hiyo imekwisha muda wake, na kwamba, Bw. Katumbi anapaswa kuomba hati mpya ya kielektroniki.
Katumbi amekuwa akiishi uhamishoni nchini Ubelgiji tangu Mei 2016, baada ya kutuhumiwa kwa ubadhirifu wa fedha katika biashara ya uwekezaji makazi na baadaye kuhukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela na pia akitumiwa kuajiri mamluki tuhuma ambazo amezikanusha .
Katumbi ambaye ni mfanyabiashara tajiri nchini Kongo, aliwahi kuwa Gavana wa Jimbo la Katanga, anatajwa kuwa kinara wa upinzani nchini humo katika uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Disemba 23 mwaka huu.

No comments