Mapipa 200 ya kemikali yanaswa Mwanza
Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa
za Kulevya (DCEA) kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na
usalama imekamata mapipa 200 sawa na lita za ujazo 50,000 ya shehena ya
kemikali bashirifu idhaniwayo kuwa ni ethyl alcohol.
Taarifa iliyotolewa na Kamishina wa
Ukaguzi na Sayansi Jinai, DCEA, Bertha Mamuya jana Desemba 22 inaeleza
kuwa kiasi hicho kilikamatwa Desemba 13 mwaka huu katika kivuko cha
Kigongo wilayani Misungwi.
Alisema kemikali hiyo ilikuwa
ikisafirishwa na kampuni ya Mwanza Lake Line Industiries kwenda mjini
Kinshasa nchini DRC Congo, ikiwa kwenye gari linalomilikiwa na kampuni
ya Mhili ya jijini Mwanza.
“Gari hili lilikamatwa likiwa halina nyaraka zinazoruhusu kisheria kusafirisha kemikali hizo,” alisema na kuongeza,
“Kitendo hicho ni ukiukwaji wa sheria
namba tatu ya kemikali za viwanda na nyumbani ya mwaka 2003, na sheria
ya dawa za kulevya namba tano ya mwaka 2015 na marekebisho yake ya mwaka
2017.”
Alisema kampuni hiyo ya Lake Line ikiwa
inatambua kuwa imekiuka utaratibu za kujihusisha na kemikali, Desemba
14, iliidanganya mamlaka ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kuomba kibali
cha kutaka kusafirisha kemikali bashirifu na kupewa kibali hicho wakati
tayari gari lenye kemikali hizo lilikuwa limeshakamatwa.
Alisema uchunguzi wa awali umeonyesha
kuwa kampuni hiyo imewasilisha taarifa za uongo katika mamlaka
mbalimbali za udhibiti, ikiwamo kiasi cha kemikali kilichokuwa
kinasafirishwa na magari yaliyotakiwa kuisafirisha.
Alisema DCEA kwa kushirikiana na
mamlaka nyingine inaendelea kufanya uchunguzi zaidi kuhusu kampuni hiyo
na kwamba uchunguzi utakapokamilika, hatua zaidi za kisheria
zitachukuliwa kwa wahusika.

No comments