Wanajeshi feki wawili wanaswa dar-es-salaam

Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam
linawashikilia watu wawili kwa tuhuma za kutumia sare za Jeshi la
Wananchi nchini (JWTZ) kufanya matukio mbali mbali ya kihalifu.
Wakati akizungumza na wanahabari jana Disemba 22, 2017
jijini Dar es Salaam, Kamanda wa Kanda hiyo, SACP Lazaro Mambosasa,
aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Lainon Fratenus (20) na Noel Cleophace
Wagesa (30) wote wakazi wa Kigogo.
“Jeshi la Polisi mnamo Disemba 15, 2017 majira ya saa
sita usiku maeneo ya Lugalo Kawe polisi wakiwa dolia walifanikiwa
kukamata wahalifu wawili wakiwa wamevalia sare za JWTZ na kisu kimoja
huku wakitumia gari namba T 306 CRU Toyota Carina rangi ya fedha,
wanatuhumiwa wanasadikiwa kujihusisha na matukio mbalimbali ya uporaji
jijini Dar es Salaam,” amesema.
SACP Mambosasa amesema watuhumiwa wanaendelea kuhojiwa
ili kubaini mtandao mzima na matukio yote waliyowahi kufanya na baada ya
upelelezi kukamilika watuhumiwa watapelekwa mahakamani kwa hatua zaidi
za kisheria.

No comments