Mfugaji tajili wa ng'ombe ambaka mtoto darasa la pili
Mkazi wa Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa ambaye ni mama mzazi wa mtoto wa kike anayesoma darasa la pili, amefikisha malalamiko yake kwa Mkuu wa Wilaya hiyo, Said Mtanda, kuwa binti yake huyo alibakwa na kuambukizwa virusi vya Ukimwi(VVU), lakini shauri hilo limefutwa mahakamani baada ya daktari kutoa taarifa za uongo.
Mtanda alieleza hayo mbele ya hadhira iliyohudhuria maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika zilizofanyika katika Mji wa Namanyere jana na kuratibiwa na Shirika lisilo la Kiserikali la Plan International unatekeleza mradi wa Kuzuia Ndoa za Utotoni katika Kata tatu za Nkandasi, Mtenga na Mkwamba wilayani Nkasi kwa ufadhili wa Wakala wa Maendeleo kutoka nchini Norway (Norad) .
“Mwezi uliopita mama mzazi wa msichana anayesoma darasa la pili alifika ofisi kwangu na kunieleza kuwa binti yake huyo alibakwa na mfugaji ‘tajiri wa ng’ombe’ ambaye amemwambukiza virusi vya Ukimwi lakini amehonga na kesi imefutwa ... Wewe hakimu, askari polisi pia daktari ambao mmemtendea hivi mtoto huyu wa kike jiulizeni je, angekuwa ni mtoto wako ametendewa hivyo ungefanyaje,” alihoji Mtanda.
Akifafanua alihoji kuwa iwapo daktari aliyemkagua binti huyo kitabibu na kutoa taarifa kuwa hakubakwa iweje mtoto huyo aanzishiwe dawa za kufubaza virusi(ARVs) .

No comments